Aika na Nahreal; Muziki Kama Kawa, Mapenzi Kama Dawa - MULO ENTERTAINER

Latest

29 Jan 2016

Aika na Nahreal; Muziki Kama Kawa, Mapenzi Kama Dawa

 Miongoni mwa wasanii wanao-ipeperusha vyema bendera ya Bongo kwa sasa ni Aika na Nahreal wanaounda Kundi la Navy Kenzo ambao pia ni ‘couple’ waliodumu kwenye uhusiano wa mapenzi kwa muda wa miaka 8, tangu waanzishe uhusiano huo mwaka 2008 walipokutana wakiwa masomoni India.
Ni ukweli usiofichika mafanikio ya wasanii hawa yanakua kwa kasi kutoka ‘uyoga’ kuelekea kuwa ‘mbuyu’, haya chini ni mambo ambayo huenda ulikuwa huyafahamu kuhusu wao.
Maisha yao binafsi
Aika na Nahreal wanakula na kupakua pamoja, akizungumzia juu ya maisha yao, Nahreal anasema imewalazimu kupanga saa za kufanya kazi pamoja na kutenga muda mwingine wa mapumziko ambao huutumia kama familia kuimarisha uhusiano wao na kutengeneza mustakabali wa maisha yao ya baadaye.
Kuhusu kazi
Wanapiga mzigo chini ya Kundi la Navy Kenzo na lebo ya The Industry inayobebwa na jina la studio wanayoimiliki, wote wakiwa mameneja mbele ya timu ya watu nane.
Kama kundi, tangu wameguke kutoka Pah One wamefanya nyimbo nyingi zikiwemo Hold Me Back, Cheza Kizembe (Waliurekodia Uganda), We Do Work, Bokodo, Aiyola, Visa na Game.
Japo hawajafanikiwa kupata tuzo lakini wameorodheshwa kwenye tuzo nyingi ikiwemo ya Top Naija Music Awards ya Nigeria pia wamewahi ‘kupafomu’ kwenye tamasha kubwa la muziki lililowashirikisha wasanii wa Kiafrika lakini wanaofanya vyema kimataifa. Tamasha hilo lilibebwa na jina la African Music Concert na lilifanyikia Afrika Kusini.
Changamoto
Nahreal anasema mwanzoni wakati wanaingia kwenye gemu changamoto kubwa ilikuwa pesa na sehemu ya kurekodia. Lakini baada ya kupata studio na muziki wao kueleweka kiasi cha kupata shoo nyingi, changamoto zote hizo zimekimbia.
Hawajawahi kutengana
Hivyo ndivyo ukweli ulivyo. Aika na Nahreal wanasema tangu waanze muziki hawajawahi kufanya kazi kila mtu kivyake, mara zote studio wako pamoja, majukwaani na kila kona wanakopiga mzigo kwenye kazi yao hiyo ya muziki.
“Unaweza kufikiri ni masihara lakini ukweli ni kwamba miaka yote sisi tumekuwa tukifuatana kama kumbikumbi linapokuja suala la kazi na hatujawahi kutengana hata siku moja,” anamaliza Nahreal.