Askari Auawa Akituhumiwa Kufanya Ujambazi - MULO ENTERTAINER

Latest

29 Jan 2016

Askari Auawa Akituhumiwa Kufanya Ujambazi

Askari polisi wilayani hapa, Nobart Chacha (25) ameuawa kwa kupigwa risasi akituhumiwa kupora mali za mfanyabiashara wa madini kwa kutumia silaha za jadi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari alisema jana kuwa askari huyo aliuawa kwa kupigwa risasi kifuani na mgongoni.

Diwani wa Kata ya Machimboni, Raphael Kalinga alisema tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana katika Kijiji cha Ibindi kilichopo Kata ya Machimboni wilayani Mlele.

Alisema askari huyo akiwa na wenzake walifika kijijini hapo kwa lengo la kumpora mfanyabiashara huyo wa madini ambaye pia anamiliki mashine za kusaga nafaka.

Kalinga alisema askari huyo na watuhumiwa wengine walivunja mlango wa mbele wa nyumba ya mfanyabiashara huyo wakati amelala chumbani.

“Baadaye waliingia ndani walimwamuru mfanyabiashara huyo kukaa kimya, lakini hakutii agizo na badala yake alichukua bunduki yake aina ya Shortgun na kumpiga askari huyo kifuani na mgongoni,” alisema.

Alisema baada ya kuona askari huyo amepigwa risasi, watuhumiwa wenzake walimchukua na kwenda kumtupa kwenye kichaka kilicho umbali wa mita 200 kutoka kwenye eneo la tukio na kisha kutoweka.

Alisema wakazi wa kijiji hicho ndiyo waliomtambua askari huyo baada ya kufuatilia michirizi ya damu na kuukuta mwili wake wake ukiwa kichakani na kutoa taarifa polisi. Alisema polisi walifika kwenye eneo hilo baada ya muda mfupi na kumtambua askari huyo.