Eliakim Maswi |
Maswi alikuwa katibu mkuu wa Wizara ya Nishati, lakini aliondolewa wakati wa sakata la uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow kwa madai kuwa hakuwajibika ipasavyo kuokoa fedha za Serikali, lakini miezi michache baadaye Ikulu ilitoa taarifa kuwa mrasimu huyo ameonekana hakukiuka maadili katika sakata hilo baada ya kuchunguzwa na Baraza la Maadili ya Viongozi.
Kauli hiyo ilifuatiwa na uamuzi wa Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kumteua kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara na baadaye Rais John Magufuli kumteua kuwa kaimu naibu kamishna wa TRA, kabla ya kumrejesha kwenye nafasi yake mkoani Manyara mapema wiki hii, akisema amemaliza kazi aliyotumwa.
Lakini wabunge na wasomi waliohojiwa na Mwananchi wamesema Rais amechukua hatua hiyo baada ya kukosolewa na wanasiasa na wadau mbalimbali wanaodai kuwa Maswi hakustahili kupewa wadhifa huo baada ya sakata hilo la Escrow.
“Amefanya hivyo kuepuka mjadala utakaojitokeza kwenye Bunge la Kumi na Moja kuhusu escrow,” alisema mbunge wa zamani wa Kigoma Kusini, David Kafulila ambaye aliibua sakata hilo bungeni mwaka 2014.
“Kuna hatari mada ya ufisadi ikaibuka kwa njia nyingine kwenye Bunge kwa kuanza kuwazungumzia hawa wahusika ambao wamerudishwa kwa namna ya pekee na kupewa nafasi nyeti,” alisema Kafulila, ambaye amefungua kesi akitaka Mahakama itengue matokeo ya ubunge na kumtangaza kuwa mshindi.
Alisema kwa nafasi aliyokuwa nayo Maswi wakati wa sakata la Escrow, hana pa kukwepea, akidai kuwa anaweza kuhusika kwa uzembe au kwa kukusudia.
“(Rais) Amemuondoa kupunguza Serikali kupingwa na wabunge kutokana na kuwabeba waliohusika na kashfa mbalimbali ikiwamo Escrow. Lakini bado kuna watu amewaacha kama (Waziri wa Nishati na Madini, Sospeter) Muhongo na (Waziri wa Katiba) Dk Harrison Mwakyembe, ”alisema Kafulila na kuongeza.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, ambaye alikuwa mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) iliyowasilisha ripoti ya sakata hilo bungeni, alisema Rais hakuwa na taarifa sahihi wakati anamteua Maswi.
Alisema hali kama hiyo ilitokea pia kwenye uteuzi wa Profesa Makame Mbarawa ambaye kwanza alitangazwa kuwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji na ndani ya siku chache akahamishiwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
“Hii inaonyesha hakuwa makini wakati anafanya uteuzi,” alisema Zitto.
“Hatutegemei kuona uteuzi wa kubadilikabadilika. Awachunguze kwa makini anaowateua na nafasi anazowapa ili kukwepa kuonekana kuwa hakuwa makini kama inavyoonekana sasa.”
Profesa Damian Gabagambi wa Chuo Kikuu cha Sokoine (Sua) aliungana na Kafulila kwamba Rais amechukua hatua hiyo baada ya kuona kasi anayoitaka, itaingia doa hasa baada ya watu kulalamikia uteuzi wa Muhongo na Maswi.
“Inawezekana wakati anamteua hakuwa akifahamu vitu vingi kumhusu (Maswi), lakini baada ya uteuzi maneno ya wadau, wasomi na watu mbalimbali yakamshtua na kufuatilia kwa umakini,” alisema.
Profesa Gabagambi alisema uteuzi wa viongozi siyo jambo dogo hasa unapotaka kuleta mabadiliko na mtazamo tofauti na uliokuwapo hapo awali.
“Unaweza kuwaona viongozi wachapakazi ambao ungeweza kuwateua, lakini kwa bahati mbaya wanatoka mkoa mmoja, hivyo ukiwateua italeta maneno. Hapo ndipo panapoleta tabu kidogo,” alisema Gabagambi.
Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ruaha (Ruco), alisema lengo la Rais Magufuli ni kujenga Serikali yenye heshima, anatamani asisikie kashfa ya aina yoyote ya ufisadi, lakini kuna baadhi ya watu inaonekana aliwateua kabla ya kufahamu kuwa wanahusika kwa namna moja aunyingine kwa kashfa hizo.
Alisema rais ana washauri ambao inawezekana walimpelekea taarifa kuhusu watu aliowateua, kazipima na kuona anaweza kuleta shida kuendelea kuwa nao hasa katika sehemu nyeti.
“Siyo kwamba Rais hasikii watu, wadau, historia ya anaofanya nao kazi inasema nini, anasikia na hilo limeonekana katika uamuzi alioufanya kwa Maswi. Ametafakari, amepima na kuona anatakiwa kufanya mabadiliko kama anataka kweli mambo yaende kama anavyotaka,” alisema Profesa Mpangala.