Msichana wa umri wa miaka 17 ambaye alikuwa katika machungu ya uzazi, amejikuta akijifungulia mtoto chooni baada ya muuguzi mmoja wa Hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam kumtaka aende kuoga na kubadilisha nguo bila ya kujali hali yake.
Msichana huyo, Asha Sudi (17), mkazi wa Tabata Kisiwani, alikutwa na tukio hilo juzi wakati akisubiri kujifungua, na uongozi wa Amana umesema utalishughulikia suala hilo.
Asha alisema alifika hospitalini hapo saa 4:00 asubuhi akiwa anaumwa na uchungu na alipofika mapokezi alikalishwa kwenye benchi.
“Wakati nikiwa nimekaa kwenye benchi alikuja nesi akaniambia niende chooni nikaoge na kubadilisha nguo. Kwa sababu sikujua, nikaenda,” alisema Asha.
Alisema akiwa chooni anajiandaa kuoga, uchungu ulikata ghafla na baada ya dakika chache aliona kitu kinaning’inia sehemu za siri kisha kikadondoka chini.
Baada ya kuona hivyo, alianza kupiga kelele akiita “nesi, nesi” na ndipo alipopita wa kwanza ambaye hata hivyo hakumshughulikia na badala yake akaendelea na kazi zake, lakini baadaye akaenda daktari ambaye hakumtambua kwa jina, akamsaidia.
“Nikiwa ninatapatapa sielewi alikuja daktari akamuokota mtoto ambaye alikuwa ameanguka chini karibu na tundu la choo,”alisema.
Baadhi ya wauguzi walitoa ushuhuda wa tukio hilo, wakiwamo daktari aliyemuokoa mama huyo na mwanaye chooni, lakini hawakutaka majina yao yatajwe
“Nilikuwa wodini. Wakati napita nikasikia mtu anapiga kelele chooni akiita ‘nesi, nesi, mwanangu jamani’. Nilishtuka, ikabidi niende kuona ndipo nikamkuta huyo binti akiwa amesima na kondo likiwa limening’inia na kitoto kichanga kimeanguka chini,” alisema.
Alieleza kuwa alikiokota kichanga hicho na mama yake kisha kuwapa huduma ya kumsafisha mtoto.
Muuguzi mwingine ambaye alikuwa zamu mchana, alisema alipopita kumuangalia mtoto huyo, alikuta akiwa na uvimbe kwenye paji la uso.
“Nikamuuliza mama wa mtoto ndipo akanisimulia. Kwanza nikashangaa huyu nesi ilikuwaje akamruhusu mama ambaye anataka kujifungua kwenda chooni?” alihoji.
Mkuu wa Idara ya Wazazi, Grace Massawe alisema wamelichukua suala hilo na kwamba watalishughulikia, lakini akawataka wazazi na ndugu wa mama huyo kuwa watulivu na kuwasamehe waliofanya tukio hilo.
“Mama tumekuelewa hili suala tutalishughulikia. Aliyefanya kosa hilo tutamuita. Najua alijisahau hasa ukizingatia bado ni mgeni, lakini tutalifanyia kazi,” alisema.
Mkuu wa Idara ya Mama na Mtoto wa hospitali hiyo, Francis Kioweli alisema mtoto huyo hajapata athari ya kiafya na kwamba endapo kutatokea tatizo lolote, basi wazazi hao wasisite kwenda hospitali kwa uangalizi zaidi.