Maalim Seif Arejea Zanzibar Akitokea India Kwenye Matibabu......Mamia ya Wafuasi wake Wampokea, Asema Polisi Imegeuka tawi la CCM - MULO ENTERTAINER

Latest

5 Mar 2016

Maalim Seif Arejea Zanzibar Akitokea India Kwenye Matibabu......Mamia ya Wafuasi wake Wampokea, Asema Polisi Imegeuka tawi la CCM

Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad jana aliwasili Zanzibar kutoka ughaibuni na kulilaumu Jeshi la Polisi nchini akisema, “hapana shaka yoyote sasa limegeuka tawi la CCM.”

Maalim Seif alisema hayo jana jioni wakati akizungumza na wafuasi wake waliofika kumpokea katika Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume na baadaye kumsindikiza hadi nyumbani kwake Mbweni mjini hapa.

Baadhi ya viongozi wa CUF waliohudhuria mapokezi hayo ni pamoja na Mansour Yussuf Himid, Nassor Ahmed Mazrui, Fatma Abdulhabibi Ferej na aliyekuwa mgombea mwenza wa Chadema chini ya mwavuliwa wa Ukawa katika urais wa Muungano, Juma Duni Haji.

Maalim Seif aliyetokea India kupitia Falme za Kiarabu, alisema anaunga mkono kauli za Mazrui ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wake, zilizosababisha ahojiwe na polisi juzi, kuwa “sasa CUF wamechoka na uhuni dhidi ya mali na ofisi zao.”

“Nasikitika kuona hujuma, watu wakipigwa na kujeruhiwa na mazombi kila kukicha, polisi wapo wanayaona na hakuna aliyeitwa kuhojiwa kwa uchochezi. Sasa haitawezekana na haitakubalika tena...” alisema.

Alipoulizwa kuhusu madai hayo jana, Inspekta Jenerali wa Polisi, Ernest Mangu alimtaka mwandishi kuzungumza na msemaji wa jeshi hilo, Advera Bulimba ambaye simu yake haikupatikana.

Hata hivyo, akizungumzia suala la mazombi hivi karibuni, Mkurugenzi wa Upelelezi Zanzibar, Salum Msangi alisema taswira ya haraka wanayoipata ni kwamba inawezekana wanaotendewa vitendo hivyo ni wahalifu ambao wamekutana na wahalifu wenzao hivyo kuhofia kutoa taarifa ili uhalifu wao usibainike hali inayosababisha kunung’unika pembeni bila ya kufikisha taarifa maeneo sahihi ili zifanyiwe kazi.

“Kwa mujibu wa taratibu zilizopo ni kwamba mtu yeyote anayefanyiwa kitendo cha kihalifu anapaswa kutoa taarifa kwenye kituo cha polisi ili hatua za uchunguzi au upelelezi zifanyike ili kubaini wahalifu hao,” alisema Msangi.

Katika hatua nyingine, Maalim Seif alimlaumu, Dk Ali Mohamed Shein kuwa si muungwana akidai kuwa amekataa kuondoka madarakani.

Alisema la kushangaza zaidi ni kuona aking’ang’ania uchaguzi wa marudio, ilihali hakuna mantiki wala kifungu chochote cha sheria kinachohalalisha hatua hiyo.

“Nasema sisi hatutambui uchaguzi huo wa marudio maana wameshindwa kututhibitishia ni wapi zilipo hizo dosari za uchaguzi uliokwishafanyika,” alisema.

Katika salamu hizo za takriban dakika 10, Maalim Seif alimtahadharisha Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha asijaribu kulazimisha chama hicho kushiriki uchaguzi ‘batili’ wa marudio.