MBOWE akosoa tamko la kamatakamata ya Rais Magufuli... Soma hapa aliyoyasema. - MULO ENTERTAINER

Latest

18 Mar 2016

MBOWE akosoa tamko la kamatakamata ya Rais Magufuli... Soma hapa aliyoyasema.

Sio wote wanaoweza kuunga mkono hotuba iliyojaa maagizo ya utendaji ya Rais John Magufuli, na mmoja wa wakosoaji ni mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ambaye amemulika matumizi ya sheria ya kuweka watu mahabusu kwa saa 48. 
Magufuli alitoa maagizo takriban sita kwa wakuu wapya wa mikoa aliowaapisha Jumanne, akiwataka wakomeshe ujambazi, kuzuia mchezo wa pool table nyakati za asubuhi, kuondoa wafanyakazi hewa, kutekeleza sera ya elimu bure, kusimamia ilani ya CCM, kuacha kupiga na kutimiza wajibu, na zaidi ya yote kuwataka kuwakamata na kuwaweka mahabusu watendaji wanaonyanyasa wananchi.
 
Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa upinzani bungeni, alisema maagizo ya mkuu huyo wa nchi, hasa ya kuwapa madaraka makubwa wakuu wa mikoa, yana kasoro na yanaweza kuchangia kuvuruga utendaji kazi na kuzua mgongano.
 
Mwenyekiti huyo wa chama hicho kikuu cha upinzani alianzia na suala la kuwapo kwa wakuu wa mikoa na wilaya, akisema ni kuendeleza mfumo wa kikoloni kwa kuwa wananchi hawakuwachagua wao kuwatumikia.
 
Alisema wananchi waliwachagua madiwani, wabunge na Rais ili wawatumikie, lakini wakuu wa mikoa na wilaya ni watu wanaopandikizwa kama ilivyokuwa wakati wa utawala wa Malkia Elizabeth wa Uingereza aliyekuwa akipeleka magavana kutawala wazalendo.
 
Sheria ya Tawala za Mikoa ya mwaka 1997 inampa mkuu wa mkoa au wilaya madaraka ya kumuweka mahabusu mtu ambaye ataona kutolala rumande kunaweza kuhatarisha amani na utulivu na hakuna njia nyingine ya kumdhibiti zaidi ya kumlaza rumande.
 
Lakini sheria inataka mtu aliyelazwa mahabusu afikishwe mahakamani ndani ya saa 48 na kama haitafanyika, aachiwe huru na asikamatwe tena kwa kosa hilo.
 
Alisema kitendo cha kuwapa wakuu hao mamlaka ya kukamata watu, kinafanya polisi wasiwe na kazi ya kufanya.
 
“Polisi watafanya kazi gani, wanasheria watafanya kazi gani,” alisema.
 
Alifafanua kuwa Sheria Namba 10 ya Serikali za Mitaa inaeleza majukumu ya madiwani liwa ni pamoja na kuwasimamia wananchi katika kila jambo, huku kukiwa na kamati maalumu za kusimamia vitu muhimu kama elimu, afya na maji.
 
Mbowe alitoa mfano wa Jiji la Dar es Salaam, ambako wananchi wamewachagua viongozi kutoka Chadema na CUF katika ngazi ya udiwani, lakini mkuu wa mkoa ni CCM, kitu ambacho alisema kitasababisha malumbano kutokana na kila upande kujiona una haki.
 
Alisema watakaokuwa huru kutimiza majukumu yao bila kuingiliwa wala kubughudhiwa na watendaji wa halmashauri ni viongozi kutoka CCM.
 
“Majiji ya Mwanza, Arusha na Dar yamekuwa yakikumbana na migogoro hii ya mwingiliano wa utendaji mara nyingi kutokana na maelekezo wanayopewa na wakuu wa mikoa,” alisema.
 
“Kibaya zaidi mikoa mingi ina wakuu ambao ni wanajeshi. Hawakufundishwa kulinda raia bali kuumiza. Kwa rungu hili, hali itakuwa mbaya,” aliongeza.
 
Mbowe aliunga mkono agizo la Magufuli la kukomesha malipo ya wafanyakazi hewa, akisema jambo hilo linapaswa kukemewa na kumalizwa kwa kuwa kutumia Sh500 bilioni kuwalipa ni kupoteza fedha nyingi.
 
Hata hivyo, alisema wafanyakazi hewa wanaozungumzwa ni wale wadogo ambao malipo yao si makubwa.
 
“Haiwezekani mkurugenzi, mhasibu au mkuu wa idara fulani akafungwa halafu isigundulike na akaendelea kulipwa mshahara,” alisema na kuongeza: “Tatizo ni uanzishaji wa mikoa, wilaya, kata, mitaa na vijiji kila utawala mpya unapoingia madarakani.”
 
Alisema suala hilo la kuanzishwa maeneo hayo ya utawala linaweza kufurahiwa na wananchi, lakini linatumia fedha nyingi, hasa za mishahara, kuongeza idadi ya watumishi wa umma na kuhitajika fedha nyingi za kuhudumia ofisi mpya. Alisema licha ya baadhi ya mambo katika hotuba kuwa na tija, mengi yana usumbufu ikiwamo utaratibu wa kufanya kazi kwa kutoa maelekezo bila kuunda mfumo wa kusimamia.
 
“Upo wapi ufanyaji usafi aliouanzisha ambao uliungwa mkono na nchi nzima. Kama angeandaa mfumo bila shaka hadi leo kungekuwa na siku maalumu ya kufanya hivyo,” alisema wakati akizungumzia uamuzi wa kufuta sherehe za Uhuru ili siku hiyo itumike kufanya usafi.
 
Akizungumzia hotuba hiyo ya maagizo, mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo-Bisimba alisema hakuna shaka kila mtu anataka vijana wafanye kazi, lakini kwa bahati mbaya hakuna ajira wala viwanda.
 
Alisema wakati wa utawala wa Baba wa Taifa vijana wasiokuwa na kazi walikuwa wanarudi vijijini wakalime kwa sababu kulikuwa na mashamba, lakini kwa sasa wamepewa wawekezaji.
 
“Badala ya kupanga kuwakusanya na kuwaweka kwenye kambi, wawaandalie maeneo ya kufanya kazi kama kuwahakikishia wale waliopoteza fedha kwenda vyuo vya ufundi ambao hawana kazi,” alisema na kuongeza:
 
“Utendaji wa sasa utasababisha Magereza kujaa kwa sababu kila mtu atataka aonekane anafanya kazi kwa kuwawajibisha wa chini yake, hali hiyo itaondoa ushirikiano katika utendaji na kuleta visasi na chuki.