Rais Magufuli Aanza Kuhujumiwa.... - MULO ENTERTAINER

Latest

8 Mar 2016

Rais Magufuli Aanza Kuhujumiwa....

SERIKALI ya Rais John Magufuli imeanza kuhujumiwa, wanaotajwa kuihujumu ni wafanyabiashara.

Wafanyabiashara wa sukari nchini wameanza kujenga utaratibu wa kuficha sukari ili kuibua malalamiko kutoka kwa wananchi lengo likiwa ni kushinikiza vibabali vya kuingiza sukari kutoka nje vinatolewa.

Hatua hiyo imemwibua Charles Mwijage, Waziri wa Viwanda na Biashara ambaye anakiri kuwepo kwa hujuma hizo na kudai, serikali haitalala.

Amesema, kuna wafanyabiashara wanaficha sukari kwenye maghala yao ili kuchochea mfumko wa bei na kisha waiuze kwa bei ya juu na hatimaye kupata faida kubwa.

Hivi karibuni Rais Magufuli alizuia kutolewa vibali holela vya uingizaji sukari nchini na kumwagiza Kasim Majaliwa, Waziri Mkuu kusimamia hilo.

Taarifa zilizopatikana zinaeleza kwamba, wafanyabiashara waliokuwa wananufaika na uingizaji wa sukari nchini wameanza kuhujumu kwa kushirikiana na wenye maghala ya sukari.

Mwijage amesema, wafanyabiashara hao wamekuwa wakificha sukari ghalani ikiwa pamoja na kufungia maghala yao ili kuzuia mfumuko wa bei na hatimaye kupata faida kubwa.

Amesema hayo katika mkutano na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam ambapo amewataka wananchi kutoa taarifa sahihi za baadhi ya watu wanaoendelea kuficha sukari kwa makusudi.

“Kama kuna taarifa sahihi za baadhi ya watu wanaoficha sukari ghalani kwa makusudi ili kuiaminisha jamii kuwa sukari ya ndani haikidhi na kupandisha bei holela ya sukari kwa masilahi yao binafsi muwataje,” alisema Mwijage.

Mwijage alisema kuwa, kwa dhamana aliyokuwa nayo katika Sekta ya Viwanda na Biashara anauwezo wa kufungia maghala yatakayobainika kuficha sukari kwa makusudi.

“Niwahakikishieni kuwa hakuna mfumuko wa bei ya sukari, mambo ni mazuri na utaratibu uko vizuri, niwasihi wawekezaji wa ndani wajitokeze kuwekeza katika viwanda vya sukari ili kuiendeleza nchi yetu,” alisema.

Alisema, Serikali inampango wa kujenga viwanda vya sukari vidogo na vikubwa ikiwemo ujenzi wa kiwanda kikubwa cha sukari kinachotarajiwa kujengwa hivi karibuni katika mkoa wa Kigoma.

“Viwanda vya sukari vinakuja,nchi yetu si ya kupokea bidhaa hafifu, sukari isiyokidhi ubora haitaingia nchini wala kuuzwa na kutumiwa na watanzania,” alisema Mwijage.