Tanzania Yatoa Ufafanuzi Kuhusu Waziri wa Nishati Wa Kenya Kuzuiwa Kuingia Bandari ya Tanga - MULO ENTERTAINER

Latest

25 Mar 2016

Tanzania Yatoa Ufafanuzi Kuhusu Waziri wa Nishati Wa Kenya Kuzuiwa Kuingia Bandari ya Tanga


Waziri wa Nishati wa Kenya, Cherles Keter, na ujumbe wake amezuiwa kuingia katika bandari ya Tanga.


Kutokana na hatua hiyo, serikali mkoani Tanga imetoa ufafanuzi kuhusu kuzuiwa kwa waziri huyo na ujumbe wake wa watu 13 kuwa kulitokana na kutokuwa na taarifa za ujio wao.


Keter na maofisa wake wandamizi wakiwamo makatibu wakuu, walijipenyeza wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati na Madini wa Uganda, Irene Muloni.


Ujumbe wa waziri huyo aliyeongozana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati ya nchi hiyo, Joseph Njoroge na mwenzake wa masuiala ya petroli, Andrew Kamau.


Vigogo hao, waliokuwa wameongozana na maofisa mbalimbali akiwamo Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mradi wa Usafirishaji wa Mafuta kutoka Lamu- Sudan Kusini- Ethiopia (Lappset), Sylvester Kasuku, walizuiwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Tanga, baada ya kuwasili.


Muloni na ujumbe wake, alitokea Kenya baada ya kukagua Bandari za Lamu na Mombasa na aliingia nchini kukagua Bandari ya Tanga, ikiwa hatua ya mchakato wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta kutoka Ziwa Albert, Uganda hadi Bahari ya Hindi.


Akizungumza hatua hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Tanga, ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa, Martin Shigella, alisema ujumbe wa Keter ulizuiwa kutokana na kutokuwa na taarifa nao na kwamba walikuwa katika viwanja vya ndege kwa ajili ya kungoja ugeni wa Waziri Muloni tu.


Shigella alisema kuwa walishangazwa kuona ujumbe huo wa Kenya umekuja kufuatana na waziri huyo bila kuwapo kwa taarifa yeyote ya awali ya ujio wao.


Keter na maofisa wake waliwasili katika uwanja wa ndege wa Tanga sambamba na ujumbe wa Waziri wa Uganda, ambao wote kwa pamoja waliwasili kwa helikopta nne, zilizotua kwa pamoja uwanjani hapo.


Baada ya kuhojiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na baada ya Waziri Muloni kumaliza ukaguzi wa Bandari ya Tanga na maeneo ambayo yametengwa kwa ajili ya ujenzi wa bomba la mafuta, iwapo mradi huo utaridhiwa kutekelezwa na serikali ya Uganda, ujumbe huo uliruhusiwa kuondoka.


Hata hivyo, serikali ya Uganda ilieleza kuridhika kwake baada ya kuona hali halisi ya mazingira ya Bandari ya Tanga ikiwa hatua mojawapo ya mchakato wa awali wa ukaguzi kabla ya kupitishwa makubaliano ya ujenzi wa mradi huo.


Kutokana na hatua hiyo, serikali hiyo inatarajia kutuma timu ya watalaamu kutoka Uganda ili kufanya ukaguzi wa kina kwenye Bandari ya Tanga, kubaini uwapo wa vigezo vinavyotakiwa katika utekelezaji wa mradi.