Yanga Yajipeleka Kwa Waarabu' Klabu Bingwa Afrika - MULO ENTERTAINER

Latest

19 Mar 2016

Yanga Yajipeleka Kwa Waarabu' Klabu Bingwa Afrika

Unaweza kusema kitendo cha wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya klabu bingwa barani Afrika timu ya Yanga ni kama wamejipeleka kwa waarabu kutokana na mchezo unaofuata kuwa ni kati yao na mshindi kati ya Al Ahly ya Misri ama Libolo ya Angola.

Mfungaji pekee wa bao la Yanga hii leo Donald Ngoma akishangilia bao lake.
Timu ya soka ya Yanga hii leo pamoja na kulazimishwa sare imefanikiwa kusonga mbele katika michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika kufuatia kuitoa APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2.

Yanga SC ikiwa katika uwanja wake wa nyumbani wa Taifa Jijini Dar es Salaam hii leo imelazimishwa sare ya bao 1-1 na timu ya jeshi la Rwanda katika mchezo wa marudiano ikiwa ni wiki moja imepita tangu timu hiyo ifanikiwe kuifunga timu hiyo ya jeshi la Rwanda nyumbani kwao Kigali katika dimba la Amahoro kwa mabao 2-1 katika mchezo wa kwanza.

Kwa matokeo hayo Yanga sasa watamenyana na mshindi wa jumla kati ya Al Ahly ya Misri na Recreativo de Libolo ya Angola katika hatua inayofuta ambapo kwa matokeo ya awali ya suluhu ya 0-0 ya ugenini huko Angola baina ya wababe hao yanatoa nafasi kwa Wamisri kuibuka kidedea na kuwakabili Yanga.

Katika mchezo wa leo, APR ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 4 kupitia kwa Fiston Nkinzingabo aliyefumua shuti kali akimalizia pasi ya Jean Claude Iranzi.
Yanga walifanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 28 kupitia kwa mshambuliaji wake, Donald Dombo Ngoma aliyefumua shuti la kitaalamu baada ya pasi nzuri ya kiungo Mzimbabwe mwenzake, Thabani Scara Kamusoko.

Kwa ujumla mchezo wa leo, Yanga walicheza kwa kujihami zaidi wakionekana dhahiri kutaka kuulinda ushindi wao wa ugenini.
Laiti kama wageni APR ingeongeza juhudi kidogo ingeweza kuwatia simanzi mashabiki wa nyumbani – lakini huenda bahati haikuwa yao kwa siku ya leo baada ya kupoteza nafasi nyingi za wazi kufuatia juhudi za washambuliaji wao kuishia kwa kukosa umakini wa umaliziaji baada ya kushindwa kutumia makosa mengi ambayo yalikuwa yakifanywa na walinzi wa Yanga.