Meneja Sober House Aanika Mazito ya Ray C - MULO ENTERTAINER

Latest

25 Jun 2016

Meneja Sober House Aanika Mazito ya Ray C

SIKU chache baada ya kufikishwa katika kituo maaulum cha kusaidia waathirika wa dawa za kulevya Bagamoyo Sober House, meneja wa kituo hicho, Godwin Msilo ameeleza mazito ya mrembo huyo sambamba na maendeleo yake kwa ujumla.

Ray C alifikishwa kwenye kituo hicho Ijumaa iliyopita baada ya kukamatwa na polisi maeneo ya Kinondoni jijini Dar akifanya vurugu baada ya kudaiwa kuzidiwa na ulevi wa madawa ya kulevya.

Akizungumza na wanahabari wetu Jumanne iliyopita katika kituo hicho, meneja huyo alisema kilichomponza Ray C hadi arudie kwenye matumizi ya madawa ya kulevya kwa mara ya pili baada ya awali kupatiwa tiba katika Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar, ni aina ya tiba hiyo kwani ilikuwa ikimpa mwanya wa kurudia kwenye matumizi ya madawa hayo.

Alisema, wao wanaamini tiba sahihi ya mtu aliyetopea kwenye madawa ya kulevya ni muathirika kufikishwa Sober House kwani wao wanamfanya muathirika asiweze kukutana na watu wengine wanaoweza kumshawishi arudie madawa hayo hatari.

Kwa mujibu wa meneja huyo, kitendo cha kumpa dawa pekee (methadone) za kumtibu muathirika wa madawa ya kulevya kisha kumuacha arejee mtaani ni tatizo kubwa lililofanyika awali kwani kilimpa mwanya mrembo huyo kujichanganya na watumiaji wa madawa ya kulevya mitaani.

“Huwezi kumtibu mtu kwa kumpa dawa halafu ukamwacha muathirika arudi nyumbani, utakuwa umemjenga vipi kisaikolojia? Kuna haja ya kumchukua muathirika kumuweka sehemu katika kituo kama hiki, anapata dawa, akishapata dawa, anapata elimu anakutana na madaktari wa afya ya akili, anakutana na madaktari wa saikolojia, wanamjenga kisaikolojia.

“Huwezi kumwacha tu, arudi nyumbani. Hujui anakula vipi, anaishije, hiyo haipo. Hivi vitu vinataka mtu ajitoe kwelikweli, apate tiba sahihi kwa kujengwa vizuri ili hata akirudi uraiani, atakuwa na uwezo mzuri wa kujisimamia mwenyewe kutokana na elimu atakayokuwa ameipata,” alisema Msilo.

Kuhusu maendeleo ya Ray C ambaye hadi Jumanne iliyopita alikuwa ametimiza takriban siku tano kituoni hapo, meneja huyo ambaye pia aliwahi kuwa muathirika wa madawa ya kulevya kabla ya kutibiwa, alisema mrembo huyo kwa sasa anaendelea vizuri.

Yeah! Ameanza vizuri tiba, anaendelea vizuri kwa kweli. Naamini kadiri anavyoendelea atakuwa vizuri zaidi. Kuna mabadiliko makubwa ameanza kuyaonesha,” alisema Msilo huku akidai muda wa kuwepo kwenye nyumba hiyo utategemeana na jinsi Ray C atakavyoonesha kupona.

Akijizungumzia yeye kama mfano wa watumiaji waliotopea na kisha kutibiwa, Msilo alisema licha ya kuwa yeye alikuwa mwanajeshi kwa muda mrefu, alijikuta ametopea kwenye madawa hayo lakini tiba pekee iliyomfanya ajinasue kwenye madawa hayo ni Sober House.

“Mimi nilikuwa mwanajeshi kwa takriban kama miaka 10 na kitu lakini nilifukuzwa jeshi kutokana na matumizi ya madawa ya kulevya, nikaenda kutibiwa Kigamboni, kwa sasa nipo freshi kabisa.

“Naomba Mwenyezi Mungu anisimamie nisiweze kurudia maana yeye ndiye anayetusaidia kuweza kufikia malengo yetu, sisi tunapanga lakini yeye ndiye anayetuwezesha,” alisema Msilo.

Kabla ya kufikishwa kituoni hapo, Ray C alipoanza kuripotiwa na magazeti ya Global Publishers kwa mara ya kwanza kuhusu kutopea kwenye madawa ya kulevya, wadau mbalimbali waliguswa na hali mbaya aliyokuwa nayo kitendo ambacho kilimgusa rais mstaafu, Jakaya Kikwete aliyemuita ikulu na kumsaidia.