Hakuna shaka kuwa menejimenti nzuri ina mchango mkubwa katika mafanikio ya msanii. Dhana hii inaweza kudhihirika kwani kuna wasanii wengi na wakubwa ambao mafanikio yao makubwa yanatokana na kuwa chini ya utawala ambao unaweza kumudu kuwasaidia kuendesha shughuli zao za kimuziki.
Kiuhalisia, menejimenti nzuri haiishii tu kupanga ni lini nyimbo itoke, ni nyimbo ipi na ya aina gani itoke, msanii apande jukwaa lipi na lipi asipande, mkataba upi asaini na upi asisaini bali pia huenda mbali zaidi na kumsaidia msanii katika kutawala maisha yake ya kila siku, kitu gani afanye na nini aseme, na pengine skendo gani aitengeneze na ipi aiepuke jambo ambalo hutengeneza mustakali mzuri katika kuhakikisha mafanikio hayaepukiki kwa msanii husika.
Kutokana na hali hii, basi ni muhimu menejimenti au lebo za muziki zikafahamu kwa undani mzunguko mzima wa sanaa na maisha ya msanii husika kabla ya kuamua kumsaini na kumsimamia. Katika kuthibitisha dhana ya kuwa menejimenti kubwa za kimataifa hazifahamu vizuri muziki wa kiafrika, mara kadhaa ambapo wasanii wamesainiwa wameishia kupoteza hata kile walichokuwa nacho.
Dbanj aliyekuwa anasimamiwa na Mo’ Hits Records chini ya Don Jazzy hakuja kuwa Dbanj aliyekuja kusaini na Good Music ya Kanye West, kwanini? Kwasababu Good Music haifahamu muziki wa kiafrika ambapo D’banj ana mashabiki wengi zaidi.
Ni dhahiri shahiri kuwa hakuna msanii ambaye asingependa kusaini kwenye lebo za menejimenti za muziki kubwa kama Sony Music Entertainment, Good Music, Roc Nation, Universal Music Group Konvict au lebo nyingine kubwa lakini pia kabla hajakata shauri la kuingia katika mkataba wa aina hiyo, anatakiwa kufikiria ni nini anakihitaji na soko la muziki wake liko wapi.
Msanii aliyeshinda Airtel Trace Muic Star 2015, shindano linalosimamiwa na kudhaminiwa na Airtel Africa na kituo cha runinga cha kimataifa cha Trace Urban kilichopo Nigeria ni kielelezo kingine kuwa lebo hizi hazitambui soko la Afrika. Mwaka mmoja baada ya kushinda shindano hilo alikuwa amefanya nyimbo moja tu chini ya menejimenti ya Universal Music Group, unafikiri ni kwanini?
Kwasababu jamaa wa menejimenti hii hawafahamu muziki wa kiafrika ni mapambano na mashindano ya kutoa nyimbo na video kali ili uweze kuwa hai kwenye kiwanda cha muziki. Mayunga ameondoka Universal Music Group, hii ina maana rahisi kuwa jamaa wamemshindwa, wameshindwana!
Jambo lingine linaloweza kuwa linaathiri ufanisi wa lebo hizi kwa wasanii wadogo hasa wa kiafrika ni kujikita na na kuweka rasilimali nyingi kwa wasanii wakubwa waliopo katika lebo hiyo. Mfano, Alikiba amesainiwa Sony Music Entertainment, je atapewa kipaumbele sawa na Davido ambaye alipewa dola milioni moja kusaini au Adele ambaye atapewa dola milioni 18 kwa mwaka? Ni wazi kuwa watajikita kule pesa ilipo.
Sony au Universal hawafahamu kabisa kuwa Mayunga au Alikiba anauza muziki wake zaidi nyumbani Tanzania au Afrika Mashariki, na si rahisi wao kuona umuhimu wa kuwasimamia katika misingi ambayo itawasaidia kukita mizizi Tanzania na kuongeza wingi wa mashabiki ambao watawafanya waonekane bara zima la Afrika, badala yake wanachukulia kama wanamsimamia Chris Brown au Justin Bieber ambaye anafahamika kila kona.
Rapper wa kike wa Uganda Keko aliichana na lebo ya Sony kabla ya kuondoka kuwa imekuwa kikwazo katika ukuaji wa muziki wake, na ni kwasababu lebo ilikuwa haimsikilizi na haitaki kutoa nyimbo zake ambazo alisharekodi wakati ambao yeye aliamini kuwa mashabiki wake walihitaji kumsikia zaidi.
Katika hali inayoonesha kuwa lebo hizi pengine huwasaini wasanii ili kujiongezea soko au umaarufu katika nchi wanazotokea, Sony ilishawahi kuwasaini Rose Muhando na Nakaaya Sumari miaka iliyopita, ingekuwa ni lebo inayotambua soko la Afrika linahitaji nini, basi bila shaka wasanii hawa wangekuwa mbali zaidi ya walipo hivi sasa.
Ni dhahiri ya kwamba muziki wa Kiafrika hauhitaji menejimentIi ya nje ya Afrika ili kufanikiwa. Miaka ya tisini kipindi muziki wa Kongo ulisikika Afrika nzima hakuna hata lebo moja ya nje ya Kongo ilikuwa ikimsimamia msanii wa Kongo bali ni watu kama wakina Logaloga ambao walifanikisha na wasanii wa Kongo wakaweza kusikika Afrika na duniani wakifanya matamasha makubwa yanayojaza viwanja Ulaya, kwanini? Ni kwa sababu tu ya kujua ni upi msimu wa Zouk, upi msimu wa Rhumba, lini na kwanini msanii aimbe lingala na lini achanganye lingala na kifaransa.
Msanii kama Wizkid anashirikishwa na msanii mkubwa kama Drake sio kwasababu ana menejimenti ya Marekani bali ni menejimentI yake ya Nigeria imehakikisha inambrand vizuri msanii wao.
Lebo kubwa kama Sony, Universal, Good Music au hata Roc Nation ni ngumu kupenya kwenye soko la Afrika labda kama uongozi wa Sony Africa ungekuwa ni wa Waafrika wenyewe, kina Don Jazzy, kina Babu Tale nk kwa sababu muziki wa Afrika una mazingira tofauti na Marekani na Ulaya.
Hapa kwetu kuna ushkaji, nani anamjua nani (wadau) na rafu za hapa na pale, sasa wale wazungu hawatambui hayo wenyewe wanachojua ni professionalism (weledi) wakati soko linahitaji weledi,fitna na figisu figisu. Hawafahamu kuna wakati msanii mkubwa anaweza akapigishwa show bure na yeye kukubali kwasababu ya kujitengenezea kesho yake(udau), hawajui muziki wa kitanzania una msimu wake wa show msanii analenga atoe nyimbo yake ili avizie msimu huo, hawajui kuna ushindani baina ya fulani na fulani hivyo msanii anaweza taka nyimbo yake itoke ili igombanie tuzo na airwaves na msanii fulani.
Kwa ushauri tu, wasanii wawe na menejimenti za ndani kwa ajili ya soko la ndani na menejimenti za kimataifa kama Sony kwa ajili ya soko la nje.