TP Mazembe na Yanga |
Tanzania tumezidi kuonekana kutofanya vizuri kwenye michezo ya kimataifa baada ya timu ya Yanga kufungwa goli 1-0 hali inayozidi kuhatarisha nafasi ya Yanga kusonga mbele kwenye hatua zijazo kutokana na kila kundi zitachukuliwa timu mbili tu zilizofanya vizuri na ndiyo zitakazoendelea hatua inayofuata.
Mchezo wa mpira daima hauhitaji siasa wa shortcut tunapaswa kujifunza sana kule walipotoka TP Mazembe mpaka kufikia hapa walipo sasa kwenye mchezo wa soka.
Haikuwa mbaya kilichofanywa na uongozi wa timu ya Yanga wa kununua tiketi na kuwagawia mashabiki wake kwa kwenda kuipa nguvu timu yao kwa kuishangilia, lakini tulijipa matumaini makubwa zaidi ya kushinda mechi ile kutokana na maandalizi tuliyoyafanya kwa mwezi mmoja pekee na kusahau kuwa TP Mazembe wameshafanikiwa kuchukuwa kombe la klabu bingwa Afrika mara tano na ndio mabingwa mpaka sasa japo wametolewa lakini bado wao ndiyo wanalo kombe hilo sasa mpaka pale watakapomkabidhi bingwa mpya.
TP Mazembe imefanikiwa kuwa na wachezaji wenye vipaji vikubwa na nguvu ya kukabiliana na timu yeyote watakayoweza kukutana nayo mbele. Sylvain Gbohoud ni golikipa namba moja wa timu ya taifa ya Ivory Coast, kepteni wa TP Mazembe, Jean Kasusula, Thomas Ulimwengu, Assane, Adam Traore, Bope na wengine wengi lakini ilikuwa ngumu kuwakutanisha wachezaji hao ambao wana uwezo wa kuamua matokeo muda wowote na wachezaji wetu ambao hawajazoea presha kubwa ya michuano mikubwa kama hiyo kutokana na kukosa uzoefu.
Kelele za mashabiki kutoka kila kona ya uwanja wa taifa haikuwa ngumu kwao kucheza kama wapo nyumbani kwa kuwa wameshazoea mara kibao kukutana na timu zenye fitina kama waarabu japo walitumia muda mwingi kwenye kujilinda na kushambulia kwa mipira mirefu ya kushtukiza.
Inapaswa kutambua kuwa TP Mazembe ni watu wanaojua namna ya kucheza mechi na siyo kuchezea mpira. Lazima ujue kuna kuchezea mpira na kucheza mechi kwa ajili ya timu kupata matokeo, hicho ndicho walichokionyesha jana Mazembe mbele ya umati wa mashabiki zaidi ya 40,000.
Ni nafasi nzuri timu ya Yanga imefika na kutambua uwezo wao waliokuwa nao kwa sasa lakini wanahitaji nguvu kubwa zaidi ya uwekezaji kwa kununua wachezaji wenye uwezo wa kupambana kwenye mashindano makubwa na siyo kuangalia wachezaji watakaoweza kushindana na timu ya Simba pekee ambao wao kwa sasa hawaangalii mashindano ya kimataifa tena zaidi ya kutolea macho vikombe vya ndani pekee.