MTU na mkewe wamenusurika kifo, baada ya nyumba yao walimokuwa wamelala kuchomwa moto na kuteketea yote.
Aliyeteketeza nyumba hiyo ni mwanamume mmoja, akidhani kuwa mke wake waliyetengana miezi kadhaa iliyopita amelala ndani ya nyumba hiyo, ili aweze kumuua.
Kamanda wa Polisi mkoani Mara, Ramadhani Ng’anzi, alisema jana kuwa tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia juzi katika kitongoji cha Mlimani eneo la Balili kona, mjini Bunda.
Alisema kuwa wazee walionusurika kifo baada ya nyumba yao kuchomwa moto ni Malenya Maduhu Suba (68) pamoja na mke Kabula (52), ambao wote ni wakazi wa kitongoji hicho.
Ng’anzi alisema siku ya tukio mwanamume huyo aliambiwa na mama mkwe wake kuwa mke wake waliyeachana naye miezi sita iliyopita na kuolewa na mwanamume mwingine yuko nyumbani kwa wazee hao amekuja kuwasalimia hao wakwe zake, ambao kwa sasa kijana wao ndiye amemuoa mwanamke huyo.
Baada ya mwanamume huyo kupata taarifa hiyo usiku wa manane aliamka na kwenda hadi nyumbani hapo na kisha kuichoma moto nyumba hiyo, akidhani kuwa mke wake ambaye tayari wameshaachana naye pia amelala ndani ya nyumba hiyo.
Aidha, alisema ndani ya nyumba hiyo kulikuwa na hao wazee wawili tu, kwani huyo mwanamke alikuwa amelala katika mji mwingine. Alisema hao wazee walinusurika baada ya kukimbilia nje, lakini wakiwa wamejeruhiwa na moto huo na kwamba kila kitu kilichokuwa ndani ya nyumba hiyo zikiwemo samani zote za ndani pamoja na kuku wakubwa 17 na vifaranga 18 vyote viliteketezwa na moto huo.
Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Francis Paul alisema wananchi walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo Mathias Masalu (26) na kumpeleka polisi. Mzee ambaye nyumba yake ilichomwa moto alisema kuwa thamani ya vitu vyote ni Sh milioni 2.5.