Rais Magufuli Asema Hatagawa Chakula cha Bure Kwa Watakaopatwa na Janga la Njaa Bila Sababu za Msingi. - MULO ENTERTAINER

Latest

1 Aug 2016

Rais Magufuli Asema Hatagawa Chakula cha Bure Kwa Watakaopatwa na Janga la Njaa Bila Sababu za Msingi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema serikali yake haitagawa chakula cha bure kwa wananchi wanaopatwa na tatizo la njaa pasipo kuwa na sababu za msingi na badala yake amewataka watanzania wajikite kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ikiwa ni pamoja na kuzalisha chakula cha kutosha.

Rais Magufuli amesema hayo jana tarehe 31 Julai, 2016 wakati akihutubia mikutano ya hadhara na kuzungumza na wananchi waliosimamisha msafara wake akiwa njiani kutoka Mkoani Tabora kuelekea Shinyanga na baadaye Geita anakoendelea na ziara yake.

Pamoja na kuwahimiza wananchi kuzalisha chakula cha kutosha ili kuondokana na njaa Rais Magufuli alisema serikali yake itajikita kuhakikisha inashughulikia tatizo la uhaba wa maji, ujenzi wa miundombinu hususani barabara na reli, kuimarisha huduma za matibabu, elimu na kutengeneza ajira.

Akiwa Isaka Mkoani Shinyanga Rais Magufuli alisema serikali haitalipa fidia kwa wananchi waliopatwa na maafa ya mafuriko yaliyobomoa nyumba zao mwezi Machi mwaka 2015 na badala yake itajielekeza kutatua tatizo kubwa la uhaba wa maji katika mji huo ambao una makutano ya reli ya kati ya kutoka Dar es Salaam kwenda nchi za Burundi na Rwanda.

Katika Mji wa Kagongwa Rais Magufuli alipokea kilio cha wananchi dhidi ya vitendo vya ujambazi na ametoa siku tano kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga kuhakikisha watu wanaojihusisha na ujambazi wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Mjini Kahama, Dkt. Magufuli aliiagiza Wizara ya Nishati na Madini kushirikiana na Mbunge wa Kahama Mhe. Jumanne Kishimba kukokotoa mahesabu vizuri na kubaini kodi ambayo Serikali inastahili kulipwa baada ya Mbunge huyo kudai kuna kiasi kikubwa cha kodi hakijakusanywa kama ambavyo sheria inaelekeza.

Aidha, Rais Magufuli alisema serikali itahakikisha wawekezaji wanaochimba madini wanaacha kusafirisha mchanga wenye madini kwa lengo la kwenda kuchakata nje ya nchi na badala yake ametaka uchakataji huo ufanyike hapa hapa nchini.

Dkt. Magufuli alizungumza na wananchi vijiji vya Segese na Bukoli na kuwahakikishia kuwa Barabara ya Kahama, Segese, Kakola hadi Geita yenye urefu wa kilometa 146 itajengwa kwa kiwango cha lami kama alivyoahidi.

Mjini Geita, Rais Magufuli alipokea kilio cha wananchi wanaodai kuwekewa zuio la kutumia mawe yenye mabaki ya madini ya dhahabu (Magwangala) kwa lengo la kusaga na kuchenjua ili kupata dhahabu, na ametoa wiki tatu kwa Wizara ya Nishati na Madini kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kufanya tathimini na kuwaruhusu wachimbaji wadogo kutumia Magwangala.

Rais Magufuli pia ameiagiza Bodi ya Pamba hapa nchini kuhamisha ofisi zake zilizopo Jijini Dar es salaam na kuzileta katika Mikoa ya kanda ya ziwa ambako uzalishaji wa zao la pamba unafanyika.

Dkt. Magufuli amewaonya viongozi na watendaji wa bodi hiyo dhidi ya vitendo vya usambazaji wa mbegu za pamba zisizoota na amesema ikitokea tena watachukuliwa hatua.

Tarehe 01 Agosti, 2016 Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli anatarajia kukamilisha ziara yake ya siku nne katika Mikoa ya Singida, Tabora, Shinyanga na Geita.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Geita

31 Julai, 2016