Polisi Wamchunguza Kamanda Sirro Tuhuma za Paul Makonda - MULO ENTERTAINER

Latest

19 Nov 2016

Polisi Wamchunguza Kamanda Sirro Tuhuma za Paul Makonda

MAKAO Makuu ya Jeshi la Polisi nchini imesema inachunguza tuhuma zilizotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda dhidi ya Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi Simon Sirro na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Kamishna Msaidizi Suzan Kaganda kuhongwa ili wasidhibiti matumizi ya dawa za kulevya aina ya shisha.

Makonda alitoa tuhuma hizo baada ya kudai kuwa viongozi hao wa polisi wamekuwa wakilegalega kusimamia ipasavyo kukomesha matumizi ya dawa za kulevya, aina ya shisha.

Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai katika makao makuu ya jeshi hilo, Kamishna wa Polisi, Robert Boaz alisema hayo jana wakati akijibu swali kuhusu hatua za jeshi hilo zilizochukuliwa kutokana na tuhuma zilizotolewa na Makonda. “..kama ilivyo taratibu zetu tunapopokea tuhuma dhidi ya kiongozi wa jeshi hili au askari yeyote tunafanya uchunguzi, kwa hiyo hata tuhuma hizi tunazifanyia uchunguzi kubaini kama ni kweli,” alisema alisema Boaz.

Wiki hii wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Umeme katika Jiji la Dar es Salaam uliofanywa na Waziri Mkuu, Makonda aliwatuhumu viongozi hao wa polisi kwa kulegalega kusimamia suala hilo huku akihofia wanaweza kuwa wamehongwa na watu waliotaka kumhonga yeye lakini akakataa.

Lakini mkuu huyo wa mkoa alienda mbali zaidi na kudai kuna kikundi cha watu 10 waliokwenda kwake ambao anawatambua kama “maajenti wa shetani” ambao wanapata faida kati ya Sh milioni 35 mpaka Sh milioni 45 kwa mwezi kutokana na dawa hizo za kulevya.

Alidai watu hao walipanga mikakati ya kumshawishi kupokea Sh milioni tano kwa kila mmoja kwa mwezi yaani Sh milioni 50 ili asipige kelele kuhusu shisha na wao waendelee kupata faida.

“Shisha imerudi katika Mkoa wa Dar es Salaam na nimeshamuagiza Kamishna Sirro, lakini nimeona kama ana kigugumizi… lakini sijajua kama hizi tano tano zimepita kwake na pia RPC wa Kinondoni nimemuona hapa, lakini hawa wana kigugumizi sijui kama hizi tano tano zimepita kwao,” alisema Makonda.

Alisema aliamua kufanya ziara mwenyewe na kushuhudia watoto wadogo wanavuta shisha. Katika suala hilo, Waziri Mkuu Majaliwa alisema atamwajibisha Makonda ikiwa hatatekeleza agizo hilo la kuondoa matumizi ya shisha katika Mkoa wa Dar es Salaam.

“Sasa mimi nasema nakuagiza wewe usimamie na kama hutasimamia suala hilo nitakuchukulia hatua, hivyo hangaika na shisha kwa wanaopuliza wakiwa wamelala hakikisha unawadhibiti,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa wakati akijibu sehemu ya salamu za Makonda alipopewa fursa ya kusalimia wananchi katika hafla hiyo.

Akijibu tuhuma hizo katika moja ya luninga nchini, Kamanda Sirro alisema mapambano dhidi ya watumiaji wa dawa hizo za kulevya za shisha yanaendelea na wameshakamata watuhumiwa wengi na kuongeza kuwa sasa kesi za wahusika wa biashara hizo ziko kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) mwenye mamlaka ya kuwafikisha mahakamani.