UWEZO wa Wanawake Kupata Mimba Washuka Tanzania - MULO ENTERTAINER

Latest

22 Dec 2016

UWEZO wa Wanawake Kupata Mimba Washuka Tanzania

Viwango vya wanawake kuweza kupata mimba nchini Tanzania vimepungua hadi 5.2 kwa kila mwanamke nchini Tanzania mwaka 2015/2016 kutoka 6.2 kwa kila mwanamke miaka ya 1991/92, kulingana na utafiti wa afya nchini humo

Kulingana na gazeti la The Citizen nchini Tanzania,utafiti huo uliofanywa na kutolewa na Afisi ya kitaifa ya Takwimu nchini humo NBS wiki iliopita unaonyesha kushuka kwa viwango vya uwezo wa kushika mimba miongoni mwa wanawake .

Kwa mfano mwaka 1996 ripoti hiyo inaonyesha watoto 5.8, mwaka 2004/05} ni watoto 5.7 mwaka 2010 ni watoto 5.4.

Utafiti huo pia ulibaini kwamba wanawake wanaoishi mashambani nchini humo wana uwezo mkubwa wa kushika mimba ikilinganishwa na wenzao wanaoishi mijini.

Gazeti hilo linasema kuwa wanawake wa mashambani wana uwezo wa kupata watoto 6 kwa kiwango cha wastani ikilinganishwa na wenzao wa mijini walio na uwezo wa kupata watoto watatu kwa wastani.

Wanawake kisiwani Zanzibar hupata watoto watano kwa kiwango cha wastani.
Ripoti hiyo pia inasema kuwa uwezo wa kushika mimba unatofautiana na elimu pamoja na hali ya kiuchumi.

Uwezo huo hupungua kulingana na kuongezeka kwa mali kulingana na ripoti hiyo, ikiongeza kuwa wanawake wanaoishi katika maeneo masikini wanapata watoto 7 ikilinganishwa na watoto 3 miongoni mwa wanawake wanaoishi katika maeneo ya kitajiri.

Ripoti hiyo pia imebaini kwamba wanawake nchini Tanzania walianza kushiriki ngono mwaka mmoja kabla ya wanaume.

Mwaka ambao wanawake huanza kushiriki ngono ni miaka 17 ikilinganishwa na wanaume ambao ni miaka 18.

Wanawake walio na elimu ya upili ama ile ya juu hushiriki ngono zaidi ya miaka mitatu baadaye ikilinganishwa na wanawake wasio na elimu ikiwa ni miaka 19 dhidi ya 16.

Takriban asilimia 14 ya wanawake na asilimia 9 ya wanaume hushiriki ngono kabla ya mwaka wa 15 na asilimia 61 ya wanawake na asilimia 47 ya wanaume hushiriki kabla ya mwaka wa 18.

Wanawake huolewa miaka miwili baada ya kushiriki ngono katika mwaka wa 19.

Vilevile gazeti hilo limesema kuwa wanawake kutoka familia za kitajiri huolewa miaka mitatu baadaye ikilinganishwa na wanawake kutoka familia masikini.