Hali si Hali,Serikali Yahaha Kutafuta Trilioni 1.7 za Kutekeleza Miradi Yake..!!! - MULO ENTERTAINER

Latest

27 Jan 2017

Hali si Hali,Serikali Yahaha Kutafuta Trilioni 1.7 za Kutekeleza Miradi Yake..!!!


SERKALI ipo katika mazungumzo na Benki ya Dunia kwa ajili ya kusaidia miradi ya maendeleo inayoandaliwa kwa mwaka ujao wa fedha itakayogharimu dola milioni 785 ambayo ni sawa na Sh trilioni 1.747.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango ameyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuzungumza na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Kanda ya Afrika, Makhtar Diop.

Dk Mpango alisema kwa upande wa kuboresha Bandari ya Dar es Salaam, mradi mzima ulikadiriwa utahitaji dola milioni 600, lakini kwa awamu ya kwanza ambayo Benki ya Dunia wamekubaliana watakwenda kuharakisha mchakato na kutoa dola milioni 305 ili kazi ianze mapema.

Alisema ipo miradi mingine ambayo ni ya kisera ambayo ni kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kufanya biashara ambayo ina thamani ya dola milioni 80 na kuna miradi mingine ambayo baada ya kumaliza majadiliano itatekelezwa.

Akitolea mfano, alisema kuna mradi wa elimu ambao utagharimu dola milioni 100, mradi wa kusaidia kuimarisha menejimenti ya bajeti na uwazi katika masuala ya bajeti ambao ni dola milioni 80, mradi wa awamu ya pili ya maji ambao ni dola milioni 100.

Dk Mpango alisema miradi hiyo inatekelezwa kwa awamu na mingine ipo kwenye maandalizi ambapo kwa upande wa makutano ya barabara uya Ubungo alisema kuwa bado hawana makubaliano ila haitapungua dola milioni 60.

Pia alisema wamelenga kuboresha sera na kufanya kuwa sehemu nzuri ya kufanyia biashara, na wamekubaliana kuongeza uwezo katika miradi ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) na kusaidia kuongeza uwezekano wa kupata wabia.