Daktari wa Macho Atoa Ushahidi Mzito ‘Kesi ya Scorpion Mtoboa Macho’...!!!
Shahidi wa nne katika kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kujeruhi
inayomkabili Salum Njwete, ameieleza Mahakama kuwa mtu aliyehusika
kumtoa macho Said Mrisho alikuwa ni mzoefu wa vitendo hivyo na siyo wa
kawaida.
Shahidi huyo, Dk Christine Mataka (52) ambaye ni daktari bingwa wa
macho kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), alitoa maelezo hayo
katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala alipotoa ushahidi dhidi ya mshtakiwa
Njwete (34) katika kesi iliyopata umaarufu wa ‘kesi ya Scorpion’
kutokana na maelezo kwamba aliyefanya uhalifu huo ni Scorpion.
Akiongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Nassoro Katuga, Dk Mataka
kutoka kitengo cha macho alidai ilikuwa mara yake ya kwanza kuona
mgonjwa aliyepelekwa Muhimbili akiwa hana vipande vya gololi za macho
yote mawili.
Dk Mataka alidai mlalamikaji Said aling’olewa macho kwa kutumia kitu
kikali kilichojikunja mbele ambacho kinaweza kutoa mboni ya jicho nzima
bila kubaki kitu chochote.
Mbele ya Hakimu Mkazi, Flora Haule alidai kwa kawaida wagonjwa
wanaopasuka jicho huwa wanakuwa na mabaki au vipande vya gololi ya
macho.