Dogo Ahaha Kumuokoa Wema Polisi,Adai Yuko Tayari Kwa Lolote kwa Kuwa Anamahaba Naye..!!!! - MULO ENTERTAINER

Latest

9 Feb 2017

Dogo Ahaha Kumuokoa Wema Polisi,Adai Yuko Tayari Kwa Lolote kwa Kuwa Anamahaba Naye..!!!!


Wakati hali ikiwa bado tete kwa Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu ambaye anashikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Kati jijini Dar, dogo mmoja anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka kati ya 12-16, aliyejitambulisha kwa jina la Hamisi Bruno, ameonekana akihaha vibaya kituoni hapo akitaka kumuokoa muigizaji huyo nyota aliyedai ni rafiki yake, Risasi Mchanganyiko lina mkanda mzima.

HIVI NDIVYO ILIVYOKUWA

Juzi Jumatatu, timu ya waandishi wetu ilipiga kambi katika kituo hicho tangu alfajiri, kwa ajili ya kutaka kushuhudia wasanii wengine waliotajwa na Mheshimiwa Paul Makonda, kwa kudaiwa kujihusisha na madawa ya kulevya wakiwasili kituoni hapo kwa ajili ya kuhojiwa.

Waliotarajiwa kuwasili ili kuhojiwa ni msanii wa Bongo Fleva, Winfrida Josephat ‘Recho’, Video Queen Tunda na staa mwingine mkubwa, Vanessa Mdee maarufu kama Vee Money.

Lakini baada ya kuwashuhudia Recho na Tunda wakiwasili kituoni hapo mapema asubuhi, kila mmoja akitegemea kumuona Vee Money, majira ya saa sita mchana, dogo huyo, alionekana kuingia kituoni hapo na kuvuta hisia za watu wengi.

ASIMAMISHWA, AWAIMBISHA POLISI

Akiwa ameweka mikono yake mifukoni na akitembea taratibu kulifuata lango la kuingilia sentro, dogo huyo alijikuta mikononi mwa polisi, waliotaka kujua wapi anakwenda na kufanya nini.

Dogo huyo aliwaambia polisi hao ambao walikuwa wameweka ulinzi mkali, kuwa alikuwa anahitaji kumuona na kumsalimia rafiki yake, Wema Sepetu na kwamba alitaka pia kuangalia uwezekano wa kumsaidia kutoka kwenye sakata hilo.

“Duu yaani huyu dogo wala hana wasiwasi, maana kuna wengine hapa watu wazima kabisa lakini hawana uthubutu kabisa wa kusogea hata pembeni ya polisi lakini yeye kaenda kukabiliana nao,” alisikika akisema mmoja wa watu waliokuwa wamejazana kituoni hapo.

ARUHUSIWA, AINGIA NDANI

Baada ya kujieleza, polisi waliokuwa wameimarisha ulinzi eneo la sentro hawakuwa na hiyana, walimruhusu kuingia mapokezi, ambapo alipoeleza pia shida yake, aliruhusiwa kwenda kumuona muigizaji huyo nyota ambaye kwa siku tano sasa, amesota rumande akituhumiwa kujihusisha na madawa hayo ya kulevya yanayomaliza nguvu kazi kubwa ya vijana wa Kibongo.

ATOKA NA CHUPA YA SODA

Dakika kumi baada ya kuwa ameruhusiwa kwenda kumsalimia rafiki yake huyo, mtoto Hamisi alitoka nje ya kituo hicho akionekana kuwa na uso wenye bashasha, huku mkononi mwake akiwa amebeba chupa tupu ya soda.

Katika hali ya kufurahisha zaidi, mtoto huyo alikataa kuzungumza, akiwapa watu ishara ya kuomba njia ili aende anakojua mwenyewe.

AREJEA…

Baada ya muda kidogo, kijana huyo aliyegeuka kuwa kivutio kituoni hapo, alirejea akiwa amebeba soda kwenye mkoba na haikuweza kufahamika ni ya aina gani, akaingia zake ndani.

ATOKA, RISASI LAMBANA

Baada ya kuingia kituoni kwa mara nyingine kwa ajili ya kupeleka soda hiyo, Risasi Mchanganyiko lilimsubiri alipotoka akiwa ameongozana na shoga mpya wa Wema Sepetu, Jike Shupa na kumtaiti, likitaka kupata mawili matatu kutoka kwake.

“Ninashukuru sana kupata nafasi ya kuonana na Wema, tena bila kipingamizi chochote, kwa kuwa ni rafiki yangu tangu 2016.

“Yaani japokuwa nina majonzi makubwa, lakini namshukuru sana Mungu, kuweza kumuona na nimempelekea soda aliyokuwa ameitaka na bado naendelea kumuombea ili aweze kutoka kwa sababu tangu akamatwe mimi sina raha kabisa,”alisema dogo huyo.