Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Prof. Mussa
Assad, imebaini kuwapo kwa matumizi mabaya ya msamaha wa kodi wa
shilingi bilioni 3.46, uliotolewa kwa walengwa wawili walioagiza jumla
ya magari 238 mwaka wa fedha wa 2015/16.
Akiwasilisha ripoti ya matokeo ya ukaguzi kwa mwaka wa fedha ulioishia
Juni 30, 2016 katika mkutano wa saba na kikao cha saba cha Bunge, Prof.
Assad amesema, msamaha huo wa kodi ulitolewa, lakini magari hayo
yalisajiliwa kwa majina ya watu tofauti na wale waliopewa msamaha.
Hata hivyo, amesema walengwa wote waliopewa msahaa huo walikana kuhusika
na magari hayo, hali inayoonyesha bado kuna uhitaji wa kuboresha
udhibiti na ufuatiliaji wa masuala ya misamaha ya kodi.
Katika udhibiti wa misahaha ya mafuta yanayoingizwa nchini kwa ajili ya
matumizi ya migodi, Prof. Assad amesema katika ukaguzi walioufanya Mei
31, mwaka jana, wamebaini lita za mafuta 4,248,802 yaliyosafirishwa
kutoka jijini Dar es salaam kati ya Oktoba 2014 na Disemba 2015 kwa
ajili ya matumizi ya mgodi wa Buzwagi, Bulyankulu na Geita, nyaraka za
uthibitisho hazikuweza kufika vituo husika na kuonesha mafuta hayo
yaliyosamehewa kodi yalitumika tofauti na makusudi.
Pia hiyo imebaini lita 20,791,072 za mafuta yenye msamaha wa kodi wa
shilingi bilioni 10.17 kwa ajili ya mgodi wa Buzwagi katika kipindi cha
miezi 18 kuanzia Julai 2014 hadi Disemba 2015, yalisafirishwa kwenda
kampuni ya M/S Agreeko mkandarasi msaidizi ambaye hakuwa mhusika wa
msamaha huo.
Kutokana na matumizi hayo mabaya ya msamaha wa kodi, Prof. Assad
ameishauri Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kufanya uchunguzi wa mafuta
yote ambayo hayana ushahidi kama yamesafirishwa vituo vya uchimbaji
madini na kukusanya kodi inayodaiwa kiasi cha shilingi bilioni 1.599 na
kodi ya shilingi bilioni 10.17 iliyosamehewa na kupelekwa kwa
wakandarasi wasiohusika na msamaha huo.
Aidha, amesema serikali inatakiwa kuhakikisha usimamizi unaimarishwa juu
ya matumizi ya misamaha inayotolewa kwa mujibu wa sheria ili kuepuka
hasara kwa serikali kutokana na matumizi mabaya ya misamaha ya kodi.