MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM), Balozi Seif Ali Iddi amemhakikishia Naibu Katibu Mkuu
wa chama hicho Zanzibar, Dk Abdalla Juma Abdalla ushirikiano wa dhati
kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake na kuona CCM inashinda katika
Uchaguzi Mkuu ujao wa 2020.
Balozi Iddi ambaye ni Mwakilishi wa
Jimbo la Mahonda alisema hayo wakati akimkaribisha katika Mkoa wa
Kaskazini Unguja Naibu Katibu Mkuu, Dk Abdalla kutokana na uteuzi wake
mpya wa kushika wadhifa huo kuongoza CCM Zanzibar.
Alisema CCM imekabidhiwa jukumu kubwa la
kupewa dhamana ya kushika dola na wananchi baada ya kuipa ridhaa
kushinda katika Uchaguzi Mkuu wa marudio ya mwaka 2016 ambao utekelezaji
wa Ilani ya CCM ni muhimu ili kutoa nafasi ya kupewa ridhaa nyingine.
Alisema Mkoa wa Kaskazini Unguja unakabiliwa na changamoto mbalimbali
ikiwemo kuwepo kwa mikakati zaidi ambayo utaifanya CCM kupambana na
upinzani.
“Tunakukaribisha katika Mkoa wa
Kaskazini Unguja ambapo tunaahidi kukupa ushirikiano wa dhati ambao
utahakikisha Chama Cha Mapinduzi kinaimarika katika mkoa wa kaskazini
Unguja ikiwemo kuingiza wanachama wengi zaidi,” alisema.
Akizungumza katika mkutano huo, Dk
Abdalla maarufu Mabodi, alisema huu ni wakati wa kufanya kazi, hivyo
viongozi wanatakiwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi pamoja na ahadi zao kwa
wapiga kura. Alisema Ilani ya Uchaguzi ndiyo makubaliano ya wananchi na
chama ambapo kwa viongozi wanatakiwa kuyasimamia kikamilifu na kuona
chama kinapiga hatua kubwa ya kuelekea katika ushindi.
Aliwaonya baadhi ya viongozi ambao
wameacha kusimamia na kutekeleza Ilani ya Uchaguzi na kwa sasa wapo
katika harakati za kupanga safu ya uongozi. “Huu si wakati wa kupanga
safu za uongozi kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa 2020... tunakabiliwa na
jukumu kubwa la kutekeleza ilani ya uchaguzi ya 2015-2020 ambayo ndiyo
makubaliano kati ya chama na wapiga kura,” alisema.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini
Unguja, Haji Juma Haji aliahidi kutoa ushirikiano wa dhati kwa Naibu
Katibu Mkuu mpya huku akiweka bayana CCM kuchukua majimbo yote ya mkoa
huo. Alisema wamejipanga vizuri ikiwemo kuingiza wanachama wapya kupitia
jumuiya mbalimbali za CCM katika hatua ya kuelekea katika Uchaguzi Mkuu
wa mwaka 2020.
“Tumejipanga vizuri sana kwa upande wa
mkoa wa kaskazini Unguja na tunaahidi kuyachukua majimbo yote ambayo
baadhi yamechukuliwa na upinzani CUF,” alisema. Majimbo mawili katika
Mkoa wa Kaskazini Unguja yamechukuliwa na CUF ambayo ni Nungwi na
Bumbwini.
19 Apr 2017
New
mulo
Habari