MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania na timu ya KR Genk ya Ubelgiji,
Mbwana Samatta, amesema anaamini timu hiyo itaibuka na ushindi nyumbani
katika mchezo wa marudiano dhidi ya Celta Vigo na kufuzu nusu fainali
ya michuano ya Europa.
Genk ilitandikwa mabao 3-2 ugenini na Celte de Vigo ya Hispania katika
mchezo wa kwanza wa michuano hiyo, hivyo inahitaji ushindi katika mchezo
wa marudiano ili kufuzu hatua ya nusu fainali.
Akizungumza jana, Samatta alisema wamefanyia kazi kasoro zilizojitokeza
kwenye mchezo wa kwanza na kusababisha wapoteze ikiwemo kupoteza nafasi
nyingi za wazi, hivyo wana matumaini ya kupata matokeo mazuri katika
mchezo wa marudiano.
Alisema anafahamu mechi ya marudiano itakuwa ya ushindani mkubwa, lakini
watalazimika kupambana kufa kupona ili waweze kushinda kwenye uwanja
wao wa nyumbani.
“Tuna matumaini makubwa ya kufanya vizuri katika mchezo wetu wa
marudiano, hivyo tayari benchi la ufundi limeanza kufanyia kazi kasoro
zilizojitokeza kwenye mchezo wa kwanza ili zisijirudie tena,” alisema
Samatta.
Samatta kwa siku za karibuni amekuwa tegemeo katika kikosi cha KRC Genk
aliyojiunganayo akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo
(DRC) aliyoichezea kwa mafanikio makubwa ikiwemo kutwaa ubingwa wa Ligi
ya Mabingwa Afrika.