Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa,
Profesa Ibrahim Lipumba ameendelea kupata pigo baada ya madiwani 18
kati ya 21 wa Mkoa wa Dar es Salaam kuungana na wabunge 40 kumpinga.
Lipumba ndani ya Bunge anaungwa mkono na wabunge wawili, Magdalena
Sakaya (Kaliua) na Maftah Nachuma (Mtwara Mjini) kati ya jumla ya
wabunge wa CUF 42, kwa upande wa madiwani wa Mkoa wa Dar es Salaam
Profesa Lipumba anaungwa mkono na madiwani wawili wa kata za Buguruni na
Kiburugwa na mmoja wa viti maalumu.
Madiwani hao wameungana kupinga jitihada za Profesa Lipumba za
kukubaliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa na uamuzi wa Wakala wa Usajili,
Ufilisi na Udhamini ((Rita) wa kuisajili Bodi ya Wadhamini aliyoiunda
na kumhakikishia kupata ruzuku ya Serikali.
Akitoa maazimio mbele ya wanahabari jana kwa niaba ya wenzake, diwani wa
Kiwalani, Mussa Kafana alisema wanaunga mkono msimamo uliotolewa na
Maalim Seif Juni 28, kupinga bodi ya Lipumba.
Kafana ambaye ni Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam, alisema Maalim
Seif alikuwa sahihi kueleza umma sababu za kutokukubaliana na hatua ya
Rita.
Alisema wanaazimia kuipinga Rita mbele ya Mahakama Kuu kwa kufungua kesi
dhidi yake kwa mujibu wa kifungu cha 26 kwa kukiuka taratibu za Sheria
za Wadhamini.
6 Jul 2017
New
mulo
Siasa