Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mh. Freeman Mbowe amelaani
kitendo cha wabunge 8 wa upinzani kukamatwa na jeshi la polisi kwa madai
yakutaka kumpiga mbunge wa CCM Juliana Shonza, na kusema hawajapeleka
mabondia bungeni.
Freeman Mbowe aliyasema hayo jana mjini Dodoma baada ya kutoka
mahakamani na kudai kuwa wao wanaamini kuwa mahakama itatenda haki kwa
wabunge hao.
"Kama ambavyo mnajua kwa masaa zaidi ya 48 wabunge wa CHADEMA wameshinda
polisi, jana siku nzima wameshinda polisi na leo wameshinda polisi
mpaka mchana huu.
"Kwa maana hiyo wawakilishi hawa wa wananchi wameshindwa kuwajibika kwa
ajili ya wananchi kwa makosa ambayo kimsingi kabisa hayakutakiwa kupewa
uzito huu yanaopewa.
"Inasemakana kuwa wabunge hawa walimfanyia fujo Mbunge wa viti maalum
(CCM) Juliana Shonza, jambo hili linafedhehesha sana, sisi tuna wabunge
ambao wanajiheshimu na kuheshimu sheria za nchi, hatukupeleka wapiganaji
bungeni bali tumepeleka viongozi wa kutunga sheria" alisisitiza Freeman
Mbowe
Mbali na hilo Mbowe anasema kitendo cha Spika wa Bunge Mh. Job Ndugai
kulivalia njuga suala hilo ni jambo ambalo yeye limemsikitisha.
"Kitendo cha kuwapeleka polisi na kuwashtaki wabunge wetu na Spika wa Bunge kushadadia jambo hili limenisikitisha sana
" Spika kusema ametoa ruhusa wahukumiwe kwa kesi za jinai ni mwendelezo
wa kutaka kutunyamazisha, ila hatutayumba na tunaamini kuwa jopo la
majaji litatenda haki katika jambo hili, maana hakuna mbunge yoyote wa
CHADEMA wala UKAWA ambaye amemshambulia mbunge yoyote yule bungeni"
alisisitiza Mbowe.
Katika watuhumiwa wote nane, mtuhumiwa mmoja ambaye ni Mbunge wa jimbo
la Ubungo, Mbunge Saed Kubenea jana alipandishwa mahakamani na
kushtakiwa kwa kosa moja la shambulio la kawaida hivyo alidhaminiwa na
shauri hilo upelelezi wake bado haujakamilika hivyo kesi itatajwa tena
tarehe 26, Julai 2017 Dodoma.
6 Jul 2017
New
mulo
MBOWE