Kuhitimishwa kwa Bunge la bajeti kumeacha kumbukumbu kumi muhimu ambazo kama ulikuwa hufuatilii kilichokuwa kikiendelea kwa siku hizo 92, leo tunakukumbusha.
Yapo mengi; yaliyofurahisha, yaliyotia simanzi na hata kufikirisha. Hayo yote yalijiri tangu Aprili 4, Bunge hilo lilipoanza mpaka jana Julai 5 lilipoahirishwa. Yalikuwapo mambo ya kisheria, kiuchumi na kijamii ambayo yaliibuka na kushughulikiwa ipasavyo na chombo hicho cha kutunga sheria.
Adhabu za wabunge
Katika Bunge hilo, adhabu ya kihistoria ilitolewa kwa wabunge wawili wa Chadema; Halima Mdee (Kawe) na Ester Bulaya (Bunda Mjini) ambao ‘wamehukumiwa’ kukaa nje ya vikao vya Bunge kwa mwaka mzima.
Adhabu hiyo ilitolewa baada ya kutiwa hatiani kwa kudaiwa kuvunja kanuni za Bunge wakati Spika Job Ndugai alipoamuru Mbunge wa Kibamba, John Mnyika atolewe nje ya ukumbi kwa kosa la kubishana naye. Katika tukio hilo, Mnyika aliadhibiwa kutohudhuria vikao vya Bunge kwa wiki moja. Kutokana na adhabu kwa wabunge wake wawili, Chadema imeliwasilisha shauri Mahakama Kuu ikiomba itengue hukumu hiyo kwa maelezo kwamba ipo nje ya uwezo wa Bunge.
Nusura wabunge wazichape
Hukumu waliyopewa Mdee na Bulaya ilichangiwa na maazimio yaliyotolewa na Mbunge wa Viti Maalumu mkoani Songwe, Juliana Shonza.
Kwa kile kinachoonekana kuwapo kwa visasi baina yao, wakati vikao vikikaribia kumalizika, wabunge wanane wa upinzani wanaidawa kumshambulia Shonza na sasa wanakabiliwa na kesi na moja wa wabunge hao wa upinzani, Saed Kubenea jana alifikishwa mahakamani kutokana na sakata hilo lililotokea Jumatatu wiki hii.
Miswada
Katika wiki za mwisho za Bunge hilo, miswada minne ilipitishwa ikiwamo mitatu iliyowasilishwa kwa hati ya dharura ambayo kwa kiasi kikubwa ilizungumzia mabadiliko ya sekta ya madini. Mmoja, ni wa sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali namba moja wa mwaka 2017, uliojadiliwa na kupitishwa jana.
Miswada hiyo imehitimisha hoja ya siku nyingi ya wapinzani waliotaka kufanyika kwa marekebisho kwenye sheria, sera na mikataba ya madini ambayo ilionekana hailinufaishi Taifa kama inavyotakiwa.
Hata hivyo, miswada hiyo iliyowasilishwa kwa hati ya dhahura, ilipingwa na kambi ya upinzani kwa maelezo kwamba muda uliotolewa haukutosha kuwashirikisha wadau wote hasa wachimbaji wadogo na wananchi waliopo kwenye maeneo yenye machimbo au migodi ya madini.
Katika mchakato wa mijadala hiyo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliweka pembeni tofauti zake na msaidizi wake mwandamizi wa zamani ambaye sasa ni Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe akimuunga mkono kuhusu hoja yake ya kutaka uwepo muundo wa uzalishaji wa madini akisema ndicho kitu muhimu cha kuzingatiwa kwenye sheria mpya.
Kamati ya Tanzanite
Wakati wa mjadala wa makadirio ya Wizara ya Nishati ya Madini, Kamati ya Nishati na Madini iliwasilisha ripoti ya ziara yake na kupendekeza kufanyika kwa mabadiliko ya usimamizi katika machimbo ya Tanzanite yaliyo chini ya Kampuni ya Tanzanite One (TML). Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dotto Biteko alisema kampuni hiyo imekuwa ikitoa taarifa za uongo na kwamba imebaini udanganyifu inaofanya dhidi ya mwekezaji mwenza, Stamico na kuiokosesha Serikali mapato stahili.
Kutokana na mapendekezo ya kamati, Spika Ndugai aliunda kamati ya watu tisa itakayoanza kazi Julai 10 kuchungua suala hilo. Kubwa litakalofanywa ndani ya siku 30 ilizopewa ni kuuchambua mkataba kati ya Shirika la Taifa la Uchimbaji wa madini (Stamico) na TML na kubainisha faida na hasara kutokana na ubia uliopo.
Pia itatathmini mfumo wa uchimbaji, usimamizi na udhibiti wa biashara ya tanzanite na inavyoweza kuchangia zaidi katika uchumi wa Taifa. Kwenye ripoti, inatakiwa kubainisha na kushauri utaratibu bora unaoweza kutumika kusimamia uchimbaji na biashara hiyo.
Kukosekana kwa Waziri wa Nishati
Tangu kutenguliwa kwa uwaziri wa Profesa Sospeter Muhongo, aliyekuwa anaongoza Wizara ya Nishati na Madini mwishoni mwa Mei, wizara hiyo imeendelea kubaki bila kiongozi.
Muhongo aliondolewa baada ya kamati iliyoundwa na Rais John Magufuli kuibua madudu kadhaa katika biashara ya madini nchini. Wakati uamuzi huo unafanywa na Rais John Magufuli, makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo yalikuwa bado hayajawasilishwa bungeni hivyo, hoja zake ama zilijibiwa na naibu waziri au mawaziri wengine.
Muswada wa fedha
Baada ya kupitisha bajeti ya Sh31.7 trilioni, Bunge pia lilipitisha Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2017 ili kuwezesha ukusanyaji wa mapato kufanikisha matumizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Katika marekebisho yaliyofanywa, wafanyabiashara wadogo wanaofanya biashara katika maeneo yasiyo rasmi wametambuliwa na kuanzia sasa watakuwa na vitambulisho rasmi.
Muswada huo pia unawagusa wachimbaji wadogo wa madini, kampuni zinazopata hasara, taasisi zisizo za Serikali (NGO), wasafirishaji wa maua nje ya nchi na wachimbaji wadogo ambao kuanzia mwezi huu, wataanza kulipa kodi. Kwenye mabadiliko yaliyopendekezwa, kodi ya majengo iliyokuwa chini ya halmashauri sasa inakusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Kutenguliwa na kuteuliwa mawaziri
Wiki moja kabla ya vikao vya Bunge kuanza, Rais Magufuli alifanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri. Alimuengua aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye na kumwingiza Profesa Palamagamba Kabudi bungeni akiwa Waziri wa Katiba na Sheria.
Profesa Kabudi alichukua nafasi ya Dk Harrison Mwakyembe aliyemrithi Nape ambaye sasa anabaki kuwa Mbunge wa Mtama.
Profesa Kabudi ndiye aliyesimamia mabadiliko ya sheria kadhaa ambazo miswada yake iliwasilishwa, kujadiliwa na kupitishwa na Bunge.
Miswada iliyopitishwa imependekeza kuvunjwa kwa Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA), kupunguzwa kwa mamlaka ya waziri wa nishati na madini na kamishna wa madini huku ikianzishwa taasisi nyingine ya usimamizi.
Mengine ni kuanzishwa kwa kamisheni ya madini itakayokuwa na wajumbe tisa, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuanza kutunza dhahabu na vito kama sehemu ya akiba ya Serikali na kuimarisha ulinzi kwenye migodi na machimbo yote na kujengwa kwa maghala na kuanzishwa kwa masoko maalumu ya madini.
Wabunge wa Chadema Eala
Miongoni mwa matukio yatakayokumbukwa katika Bunge safari hii ni mshikemshike wakati Bunge lilipowachagua wabunge tisa kuliwakilisha Taifa, Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (Eala).
Hata hivyo katika uchaguzi wa kwanza, majina mawili yaliyowasilishwa na Chadema; Ezekeah Wenje na Lawrence Masha yalipigwa chini baada ya kuzidiwa na kura nyingi za ‘hapana’.
Hata hivyo, chama hicho kilipopeleka majina kwa mara ya pili, waliochaguliwa kuhitimisha idadi ya wabunge tisa ni Josephine Lemoyan na Pamela Massay.
Awali, wabunge waliochaguliwa kuiwakilisha Tanzania kwa upande wa CCM ni Fancy Nkuhi, Happines Legiko, Maryam Ussi Yahya, Dk Abdullah Makame, Dk Ngawaru Maghembe na Alhaj Adam Kimbisa. Kwa upande wa CUF ni Habib Mnyaa.
Makinikia
Baada kukabidhiwa kwa ripoti ya pili ya uchunguzi wa usafirishaji wa mchanga wa dhahabu nje ya nchi na kamati ya Rais, mjadala mkubwa wa makinikia ulitawala bungeni.
Ripoti hiyo iliyowasilishwa Juni 13, ilibainisha upungufu kadhaa kwenye mkataba wa kampuni ya Acacia inayochimba na kumiliki dhahabu kwenye migodi ya North Mara, Bulyanhulu na Buzwagi. Moto uliongezeka zaidi baada ya Mwenyekiti ya Kampuni ya Barrick Gold inayoimiliki Acacia, Profesa John Thornton kuja nchini na kukutana na Rais Magufuli na kukubali kufanya mazungumzo ili kupata muafaka wa sakata hilo.
Acacia wamewasilisha mgogoro huo na Serikali kwenye mahakama ya usuluhishi.
Kamati ya almasi
Spika wa Bunge, Job Ndugai jana aliunda Kamati Maalumu ya ushauri kuhusu mfumo wa usimamizi, umiliki na udhibiti wa madini ya almasi ambayo inajumuisha wabunge tisa.
Kamati hiyo itaongozwa na Mbunge wa Ilala (CCM), Mussa Azzan Zungu. Akitangaza kamati hiyo muda mfupi kabla ya kuahirisha Bunge jana, Spika Ndugai alisema aliiteua kwa kuzingatia vigezo vya taaluma, uzoefu, pande za Muungano, jinsia na uwakilishi wa vyama vya siasa bungeni.
Alisema itakapobidi, kamati hiyo itafanya ziara katika maeneo mbalimbali kwa kuzingatia muda wake wa kazi, bajeti na ulazima wa kufanya hivyo.
“Katika kutekeleza majukumu yake, kamati itashauriwa kwa karibu na sekretarieti itakayoteuliwa na Katibu wa Bunge,” alisema Ndugai.
Aliwataja wajumbe wa kamati hiyo kuwa ni Dk Immaculate Sware (Viti Maalumu - Chadema), Shally Raymond (Viti Maalumu – CCM) na Rashid Ali Abdallah (Tumbe - CUF).
Wengine ni Allan Kiula (Iramba Mashariki - CCM), Restituta Mbogo, (Viti Maalumu -CCM), Ahmed Juma Ngwali, (Ziwani - CUF), Richard Ndassa ( Sumve – CCM) na Emmanuel Mwakasaka (Tabora Mjini - CCM).
“Kamati hiyo itafanya kazi kwa muda wa siku 30 kuanzia Julai 10, 2017. Kituo kikuu cha kazi kitakuwa katika Ofisi ya Bunge hapa Dodoma,” alisema.
Hadidu za rejea za kamati hiyo ni kuchambua taarifa za Tume na Kamati mbalimbali zilizowahi kuundwa na Serikali kwa ajili ya kushughulikia mfumo wa uchimbaji, usimamizi, umiliki na udhibiti wa madini ya almasi nchini na kuona mapendekezo yake na namna yalivyotekelezwa na Serikali.
Nyingine ni kutathmini mfumo uliopo wa uchimbaji, usimamizi na udhibiti wa biashara ya madini ya almasi nchini na kubainisha manufaa ambayo Serikali inapata kutokana na uwekezaji uliopo.
Nyingine alisema ni, “Kubainisha na kushauri kuhusu utaratibu bora unaoweza kutumika katika kusimamia uwekezaji, uchimbaji na biashara ya madini ya almasi nchini.”
Alisema kamati hiyo itatathimini mfumo wa uchimbaji, usimamizi, umiliki na udhibiti wa madini ya almasi nchini kisha kuandaa mapendekezo kwa ajili ya kuishauri Serikali kuhusiana na uendeshaji bora wa biashara ya madini hayo nchini. Alisema uamuzi huo umetokana na Rais John Magufuli kupendekeza Bunge liunde kamati ya kuchunguza na kufuatilia madini hayo.