Dodoma Pamenoga Leo Uchaguzi Mkuu TFF - MULO ENTERTAINER

Latest

12 Aug 2017

Dodoma Pamenoga Leo Uchaguzi Mkuu TFF


Dodoma Pamenoga Leo Uchaguzi Mkuu TFF
Shughuli ya Uchaguzi Mkuu wa TFF imeanza mkoani Dodoma ambapo wajumbe kutoka mikoa tofauti hapa nchini wameanza kujitambulisha.


Tangu jana mjini hapa kumekuwa na heka heka kwa wajumbe na wagombea kuhakikisha kambi zao zinapata kura nyingi kuelekea katika uchaguzi huo.

Wagombea wengi mpaka kufiki jana walikuwa wako bize kuomba kura kwa wajumbe ikiwa jana ilikuwa siku ya mwisho wa kampeni.

Hata hivyo, hadi kufikia jana hakuna mgombea ambaye alikuwa na uhakika wa nani anachakua nafasi ya Jamal Malinzi katika nafasi hii ya urais.

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na mwandishi wetu jana, ulionyesha Wallace Karia na Ally Mayayi walikuwa wakipewa nafasi kubwa katika nafasi ya urais.

Mmoja wagombea wa nafasi ya Urais, Fredrick Mwakalebela, aliliambia Nipashe kuwa kwa sasa jukumu limebaki kwa wajumbe huku akijipigia upatu kuwa yeye ndiye mtu sahihi wa kuiongoza TFF.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa TFF, Revaocatus Kuuli, aliliambia Nipashe kuwa mpaka kufikia leo mchana majibu ya nani amekuwa kiongozi wa TFF yatakuwa yamepatikana.

“Uchaguzi utakuwa wa haki na halali kwa kila mgombea, tutampata mtu ambaye atakuwa amechaguliwa na wajumbe,” alisema Kuuli.

Alisema Kamati yake inasimama kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa haki na kwa yeyote atakayekiuka kanuni ya uchaguzi chombo husika, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru), itafanya kazi yake.