Maswali mazito yameibuka juu ya uamuzi wa Serikali kuwarudisha kazini
kimyakimya wajumbe saba wa bodi na watendaji waandamizi wanne wa Baraza
la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), siku chache baada
ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira),
January Makamba, kuwasimamisha.
Mwananchi limedokezwa kuwa hivi sasa watumishi hao, akiwamo Kaimu
Mkurugenzi Mkuu, Vedasto Makota wanaendelea na kazi zao kama kawaida kwa
maelekezo ya mamlaka za juu.
Wiki mbili zilizopita, Makamba alitangaza kutengua uteuzi wa wajumbe
saba wa Bodi ya NEMC na kuwasimamisha wakurugenzi wake wanne ---Manchare
Heche, Deus Katwale, Andrew Kalua na Benjamin Dotto--- kwa tuhuma
kadhaa ikiwamo ya ucheleweshaji wa vibali vya ukaguzi wa mazingira na
tuhuma za rushwa.
Alisema NEMC ina upungufu mkubwa kiutendaji huku akiwatuhumu baadhi ya
watendaji kwa kuwasaidia watu wenye masilahi nao na kushindwa kutoa
maelezo ya kuridhisha pale walipotakiwa kufanya hivyo.
“Kulingana na mamlaka niliyonayo chini ya Sheria ya Mazingira Kifungu
cha 19 (2), nimeamua leo kutengua uteuzi wa wajumbe wote saba wa Bodi ya
NEMC ili baadaye niteue wajumbe wapya ambao wataenda na kasi na ari
tunayoihitaji sasa katika kuelekea uchumi wa viwanda. Mwenyekiti wa
Bodi, ambaye mamlaka yake ya uteuzi ni Mheshimiwa Rais, ataendelea
kuwepo hadi Mheshimiwa Rais atakapoteua mwingine.”
Pia alisema, “Tumewasimamisha kazi baadhi ya watendaji wa NEMC kuruhusu
uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazowakabili kabla ya kuchukua hatua zaidi.”
Makamba alimteua Dk Elikana Kalumanga kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NEMC.
Hata hivyo, baada ya hatua hiyo, imeelezwa kwamba wote walioondolewa
wamerejeshwa kimyakimya. Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Vedasto Makota
hakupatikana kuzungumzia suala hili na mmoja wa waliosimamishwa kazi,
Heche hakukataa wala kukubali kwamba amerudishwa kazini, akisema hawezi
kuzungumzia suala hilo kwa kuwa liko chini ya mamlaka ya waziri.
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa tangazo hilo la Makamba halikudumu
kwa zaidi ya wiki moja baada ya mamlaka za juu kuagiza hali irudi kama
ilivyokuwa awali.
Baadhi ya watu walio ndani ya NEMC wamedai kuwa uamuzi huo wa Serikali
utaathiri kwa kiasi kikubwa utendaji wa Baraza hilo la Mazingira
linalokabiliwa na changamoto nyingi kiasi cha mchango wake katika
masuala ya uhifadhi wa mazingira kuhojiwa mara kwa mara.
“Hapa palishageuka kama himaya ya watu fulani tu. Hakuna kinachoenda.
Malalamiko ni mengi kutoka jumuiya ya wafanyabiashara na wenye viwanda.
Sio siri tena kwamba rushwa imetawala hasa katika eneo la utoaji vibali
vya mazingira,” alisema ofisa mmoja wa daraja kati wa NEMC kwa sharti la
kutotajwa jina.
“Kuna ukiritimba mkubwa kutoa cheti cha mazingira na mtu kama akiwa
tayari kutoa pesa anapata hata ndani ya siku mbili tu. Kama huna
utasumbuka sana,” alisema ofisa huyo.
Wizara ya Viwanda na Biashara imewahi kusikika mara kadhaa ikilalamikia
ucheleweshaji wa utoaji wa vibali vya mazingira kama moja ya mambo
yaliyozorotesha jitihada za Serikali za ujenzi wa viwanda nchini.
Akiwa katika ziara ya kikazi Mkoa wa Pwani mwezi uliopita, Rais John
Magufuli alionyesha waziwazi kukerwa na ucheleweshaji wa vibali vya
mazingira unaofanywa na NEMC na alizungumzia suala hilo mara mbili
katika mikutano yake ya hadhara.
Mbali na ucheleweshaji wa vibali vya mazingira, rushwa inatajwa
kukithiri ndani ya wakala huyo wa mazingira huku watendaji wakidaiwa
kuwatoza faini wenye viwanda kinyume cha sheria na wakati mwingine
kuwatisha ili watoe rushwa kwa ahadi ya kuwapunguzia faini.
Akitoa mfano, ofisa mwingine wa NEMC aliyeomba kutotajwa jina amesema
baadhi ya maofisa waliwahi kukitoza kiwanda cha kuchinja nyama ya punda
mjini Dodoma kinachomilikiwa na raia wa China faini ya Sh240 milioni
kinyume na Sheria za Mazingira.
Suala hilo linadaiwa kufika mezani kwa waziri Makamba ambaye baada ya
uchunguzi na kuweka vielelezo mezani zikiwamo risiti za tozo,
ikagundulika wawekezaji hao walilipa Sh20 milioni tu huku watu wa NEMC
wakiondoka na Sh100 milioni baada ya kukubali kuwapunguzia Wachina hao
kiasi cha faini.
Ofisa huyo alidai kuwa watendaji hao waliamua kughushi mukhtasari kuonyesha kwamba mwekezaji huyo aliomba kupunguziwa faini.
Taarifa zinasema kuwa watendaji wote wa NEMC waliotajwa kwenye
mukhtasari huo baada ya kubanwa walikikiri kuwa hawakuhudhuria mkutano
uliozaa mukhtasari huo na kwamba hawana mamlaka ya kumpunguzia mtu faini
isipokuwa waziri peke yake.
Mtoa taarifa wetu anadokeza kuwa hata bodi ilipofikishiwa suala hili ikasema watu hao wapewe onyo wakati kosa ni la wazi kabisa.
“Huku ni kulindana tu na NEMC isipokuwa overhauled (fumuliwa)
tusitegemee chochote. Hizi ni zama za accountability (uwajibikaji) na
kwa kweli kuna mambo hayaendi sawa humu mwetu. Sisi tukiboronga madhara
kwa nchi ni makubwa kuliko watu wanavyoona,” alisema ofisa huyo wa NEMC.
Alipotafutwa kwa simu, waziri Makamba alikataa katakata kuzungumzia
suala hilo. “Sisi tuko vizuri tu na tunatekeleza mipango ya Serikali
kama kawaida. Sina zaidi ya hilo,” alisema.
Habari kutoka ndani ya wizara zinasema kukithiri kwa matatizo ndani ya
NEMC kuliwahi kumsukuma Waziri Makamba kuwaita watendaji wake na kuandaa
mkakati wa kuyashughulikia, wakilenga zaidi suala la utoaji vibali vya
mazingira kwa kuangilia muda unaotumika kwa kazi hiyo, gharama na kuziba
mianya yote ya rushwa.
Vyanzo vyetu vinasema kuna wakurugenzi ambao wanakabiliwa na tuhuma za
wazi za kukiuka sheria za utumishi wa umma ikiwamo rushwa na ndizo
zilizomsukuma Waziri Makamba kuwasimamisha kazi akijipanga kufanya
mabadiliko makubwa ndani ya NEMC.
Watu wanaofuatilia kwa karibu sakata hili wanasema makundi yenye
masilahi ya kiuchumi na NEMC hawakupendezwa na mwelekeo wa Makamba
katika kuifumua NEMC ndipo wakaanza mkakati wa chini kwa chini
kukabiliana naye.
Makundi hayo ndiyo yanayodaiwa kuiteka NEMC na yanalaumiwa kwa
kukwamisha juhudi mbalimbali za wizara na Serikali kwa miaka mingi sasa
kama vile kuzuia matumizi ya mifuko ya plastiki na kudhibiti viwanda
dhidi ya uchafuzi wa mazingira na kujenga jumba za kifahari ndani ya
hifadhi za fukwe mbalimbali.
Haijulikani ni nani, katika mazingira gani na kwa sababu ipi aliamuriwa
‘kumzima’ Waziri Makamba lakini vyanzo vyetu ndani ya NEMC vinaonya kuwa
uamuzi huo utaadhiri utendaji kazi wa baraza na kumpunguzia waziri
mamlaka ya kiutawala dhidi ya Baraza hilo.
Habari zinasema tayari Wangwe, alikwishapewa barua ya kuondolewa NEMC na kurudishwa Hazina.
Wafuatiliaji wanahoji pia ni jinsi gani Makamba atapeleka uso wake na
kuanza kufanya kazi na kundi la watu ambao hana imani nao tena na
alikwishaamua kuwaondoa kazini.
“Huu uamuzi sijui umechukuliwa na nani lakini jambo lililo wazi ni
kwamba utamuondolea kabisa waziri moral authority (mamlaka ya kimaadili)
kutimiza mipango yake na watu hawa waliorudishwa. Hali hii nina hakika
imemshushia hadhi hapo wizarani na itakuwa imemvunja sana moyo,” alisema
mtoa taarifa huyo.
Wadadisi pia wanahoji endapo mikakati iliyopo ya kuifumua NEMC na
kuifanya ifanye kazi kwa ufanisi na uadilifu zaidi itatekelezwa katika
mazingira ya sasa.
Kwa upande mwingine, suala hili kwa namna moja au nyingine limeiweka
majaribuni vita ya Rais Magufuli dhidi ya rushwa na utendaji usioendana
na kasi yake hasa ikizingatiwa hata aliwahi kuonyesha kutoridhishwa na
ufanisi wa NEMC.
“Tatizo ni wazi kabisa hawa watu walishafeli kabisa katika majukumu na
Makamba aliona ili mambo yaende lazima awaondoe. Sasa changamoto kwa
huyu bwana (Makamba) ni kuhakikisha kazi na mipango yake vinaendelea
katika hali ya vikwazo vilivyo mbele yake,” anasema.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema inawezekana waziri huyo kijana
hakufanya mawasiliano ya kutosha kabla ya kuchukua uamuzi wake.
“Hili haina tafsiri nzuri. Nchi nyingine waziri huwa anajiuzulu kwa
sababu mamlaka yake yamevizwa. Inawezekana alichukua hatua hiyo bila
mawasiliano ya kutosha. Sidhani kama walimpa go ahead (ruhusa) halafu
wa-reverse (wageuke),” anasema Profesa wa Chuo Kikuu Katoliki cha Ruaha
(RUCU), Gaudence Mpangala.
“Unajua mfumo wa utawala wetu wa sasa walio chini ya Rais mara nyingi
wanachukua hatua kwa kudhani wanampendeza Rais au waonekane wanafanya
kazi lakini si mara zote hiyo inafanya kazi.”
Profesa wa Sayansi ya Siasa, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Benson Bana
alisema hatua ya Serikali kubadili uamuzi ya Makamba inaashiria kuwa
hakufanya mawasiliano ya kutosha kabla ya kuchukua uamuzi wake.
“Nafikiri inawezekana ni tatizo la mawasiliano na mamlaka. Unajua
kimsingi Makamu wa Rais ndiye mwenye dhamana. Waziri hana instruments.
(mamlaka). Sasa kuvunja bodi ni dhamana ya Makamu wa Rais. Swali kubwa
la kujiuliza hapa ni je, Makamu wa Rais alijulishwa na kuridhia mpango
wa Makamba? Kama hakuridhia inawezekana ndiyo sababu mambo yamekuwa
hivyo,” alisema Bana.
Source: Mwananchi
7 Aug 2017
New
January Makamba Abaki njia Panda Baada ya Watu Aliowafukuza Kazi NEMC Kurudishwa Kazini Kinyemela
mulo
Makamba