Msanii wa muziki wa bongo fleva Q Chief ambaye hivi karibuni ameachia
ngoma yake mpya ya 'Naogopa', amezungumzia suala la kubadili dini na
kuingia kwenye dini nyingine, baada ya kuwa karibu na mchungaji Anthony
Lusekelo.
Akizungumza na mwandishi wa East Africa Television, Q Chief amezungumzia
suala hilo na kusema huwa familia yake upande wa mama ni Wakristo na
ana amini katika Mungu, lakini sio rahisi kwake kubadilisha imani yake.
"Familia yangu upande wa mama wengi ni wakristo, lakini wamegawanyika
kutoka kwenye uislam kwenda ukristo, baba yangu ni muislam, babu yangu
ana msikiti kwa hiyo sio jambo jepesi kutoka kwenye dini yangu imani
yangu kwenda kwenye imani nyingine, naamini Mungu ndiye jibu sahihi,
lakini huwa nachukua ushauri wa viongozi wa dini tofauti tofauti",
alisema Q Chief
Q Chief aliendelea kwa kuzungumzia kitendo chake cha kuwa karibu na
Mchungaji Anthony Lusekelo 'Mzee wa Upako', na kusema Mchungaji huyo ni
sawa na kaka yake na anapenda anavyomshauri.
"Kuna siku moja nilipigiwa simu usiku kama saa saba hivi, kupokea ni
Mzee wa Upako nikashtuka, nikasema kuna kitu gani au zali
zimenindondokea! lakini nikagundua ni shabiki yangu namba moja, na siku
zote amekuwa akitamani kunishauri, kunijenga kiimani lakini pia
kuzungumza na mimi kama kijana, kwamba lolote unalopitia usisahau Mungu
amekuweka kwa sababu, na Mungu yupo kuwainua wale walioanguka, naheshimu
ushauri wake kama kiongozi, kama kaka mshauri kama mchungaji", alisema Q
Chief.
7 Aug 2017
New