Waziri Majaliwa Awataka Watendaji Kuwafuata Wananchi na Si Kukaa Ofisini - MULO ENTERTAINER

Latest

15 Feb 2018

Waziri Majaliwa Awataka Watendaji Kuwafuata Wananchi na Si Kukaa Ofisini

Waziri Majaliwa Awataka Watendaji Kuwafuata Wananchi na Si Kukaa Ofisini


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewaagiza wakuu wa wilaya na watendaji wa halmashauri kutoka maofisini kuwafuata wananchi maeneo yao ili kusikiliza kero zao.

Amesema hayo leo Februari 15, 2018 katika Ikulu ndogo jijini Mwanza baada ya kupokea taarifa ya mkoa huo na kuzungumza na viongozi mbalimbali wa Serikali na dini.

"Watendaji hamna sababu ya kukaa ofisini wakati wananchi wanahangaika na kero, nendeni kwa wananchi kwa kuwa wao hawana uwezo lakini nyie mnawezeshwa kila kitu,” amesema Majaliwa.

Pia, Majaliwa ameagiza watendaji wa halmashauri kuhakikisha wanakuwa na Ilani ya CCM, kuisoma na kuielewa hata kama mtendaji atakuwa sio kada wa chama.

Pia, ameagiza kufanya operesheni kuhakikisha mipaka ya Ziwa Victoria inalindwa kwa kuwahoji watu wote ambao watakuwa na mashaka nao,  si kufanya operesheni ya  uvuvi haramu pekee.

Majaliwa amesema lengo la ziara yake ni kukagua huduma muhimu za afya, maji, elimu na miundombinu  kwa kuwa Serikali inahitaji kuona wananchi wanapata mabadiliko makubwa katika maendeleo.

Amesema kwenye ziara yake atatembelea mashamba ya pamba kujionea maendeleo na kuzungumza na wakulima, lengo la Serikali ni kufufua zao hilo na jitihada zimeanza.