Breaking News: Rais Magufuli Afunguka Mambo Mazito Sakata la Dhahabu ya Mamilioni ya Pesa Iliyonaswa Jijini Mwanza - MULO ENTERTAINER

Latest

9 Jan 2019

Breaking News: Rais Magufuli Afunguka Mambo Mazito Sakata la Dhahabu ya Mamilioni ya Pesa Iliyonaswa Jijini Mwanza


Rais Magufuli amempongeza Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania-IGP Simon Sirro  kwa kuhakikisha watuhumiwa wote wa Dhahabu ya mamilioni ya pesa iliyokuwa inatoroshwa jijini Mwanza wamekamatwa wakiwemo Askari polisi 8.


Rais Magufuli ametoa pongezi hizo Leo Jumatano January 9, 2019  Ikulu Dar es Salaam wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua jana.


Akisimulia kwa kina kuhusu tukio hilo, Rais Magufuli amesema watuhuhiwa hao walikamatwa January 4 Misungwi, kisha wakarudishwa kituo kikuu cha kati, lakini hawakuwekwa Mahabusu.


"Kwa taarifa nilizonazo, watuhumiwa wale walishikwa Januari 4, wilayani Misungwi, wakarudishwa mjini Mwanza na Kikosi cha Polisi nane, wakawapeleka Central wala hawakuwaingiza ndani, watuhumiwa walikuwa kwenye gari, wakawa wanajadili namna ya kuwapa hela, wakawaambia watawapa Bilioni 1 "  Amesema Rais Magufuli


Amesema, watuhumiwa hao walitoa Rushwa ya milioni 700, ikawa imebaki milioni 300 ambayo polisi hao waliahidiwa kwamba watapewa wakifika Sengerema.


Rais Magufuli ameendelea kusimulia kuwa, usiku huo  watuhumiwa waliondolewa Central  huku wakisindikizwa na Polisi hao kuelekea Sengerema.

“Askari  Polisi hao waliendelea kuzunguka na watuhumiwa hao  kwa kutumia magari na mafuta ya Serikali, wakavuka Kigongo Ferry kuelekea Sengerema. "Amesema Rais Magufuli


Rais amesema taarifa za kiintelijensia zikawa zimemfikia, akatoa maelekezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwamba watu hao wafuatiliwe haraka na wakamatwe.

"Niliwasiliana na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella na Mkuu wa Wilaya ya Sengerema ili wakamatwe, iliwekwa road block na wakakamatwa. Askari wale wakaanza kupiga king’ora eti walikuwa wanawafukuza kumbe walikuwa wanawasindikiza. "Amesimulia Rais Magufuli.


“Nakupongeza sana IGP kwa kuwashughulikia askari hao, tena huyo Superintendent wa Polisi aliyekuwa akisindikiza huo mzigo umemvua cheo, na watapelekwa kwenye mahakama za kijeshi kisha mahakama za kiraia,” Amesema