Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan Akerwa Makusanyo kidogo ya Kodi Singida.....Atoa Maagizo Mazito - MULO ENTERTAINER

Latest

17 Feb 2019

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan Akerwa Makusanyo kidogo ya Kodi Singida.....Atoa Maagizo Mazito


Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amewaagiza watendaji wa Mkoa wa Singida kuhakikisha wanajiimarisha kikamilifu katika ukusanyaji mapato ya ndani kwenye halmashauri zao ili kuleta maendeleo ya kweli kwa watu wake.

Amesema hayo baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji ya mkoa mjini hapa kutoka kwa Mkuu wa Mkoa, Dk Rehema Nchimbi, iliyoonesha kuwa wastani wa makusanyo ya mapato kwa mkoa huo kwa sasa ni asilimia 39 tu.

“Makusanyo ya mapato yenu ni aibu tupu. Wakati wenzenu wanakusanya zaidi ya asilimia 80 ninyi mnakusanya asilimia 39 tu. Mnasubiri wenzenu wakusanye ninyi mje mgawiwe,” amesema Makamu wa Rais.

Ameongeza: “Huu ni unyonyaji. Tumieni vyanzo vyenu mbalimbali vya mapato ili kujiletea maendeleo yenu na ustawi wa wananchi wenu.”

Akitolea mfano wa mapato yanayoweza kupatikana kwa kuuza kuku, Makamu wa Rais amesema kutokana na taarifa kuonesha kuwa mkoa huuza kuku zaidi ya 23,000 kwa siku, hata kama watatoza ushuru wa Sh mbili kwa kila kuku bado mkoa utakusanya mapato ya kutosha.

Aidha, alikemea tabia ya ubadhirifu na udokozi wa fedha za miradi mbalimbali ya afya na kuagiza pawepo na usimamizi wa karibu kwa miradi yote ya afya.

“Nia ya serikali katika kujenga vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya, ni kupunguza vifo vya akinamama na watoto nchini. Hivyo, ni lazima miradi hiyo isimamiwe kikamilifu,” amesema.

Makamu wa Rais amewataka viongozi wa ngazi zote mkoani Singida kuondoa tofauti zao za kiutendaji vinginevyo hawataendelea kuvumiliwa.

“Taarifa za ulinzi na usalama za mkoa zinaonesha mahusiano baina ya baadhi ya viongozi na watendaji hapa kwenu zinaonesha hamko vizuri. Kila mmoja ana eneo lake la kazi, sasa mnachogombania ni nini?” amehoji.

Aliwataka kila mmoja wao kujitathimini kutokana na ukweli kwamba bila maelewano, mambo hayawezi kwenda vizuri ndani ya mkoa.

Awali, akisoma taarifa ya mkoa mbele ya Makamu wa Rais, Dk Nchimbi alikiri Singida hadi sasa umekusanya kiasi cha asilimia 39 tu ya mapato huku akisema “kwa kweli mkuu hatufanyi vizuri hata kidogo. Hatuna majibu zaidi ya hayo.”

Makamu wa Rais jana alitembelea shamba la korosho la Masigati lenye ukubwa wa ekari 26,000 kabla ya kumaliza ziara yake wilayani Manyoni kwa kutembelea Halmashauri ya Itigi. Leo anaendelea na ziara Wilaya ya Ikungi.