DC Katambi akutana na Harmonize, wafanya mazungumzo mazito - MULO ENTERTAINER

Latest

17 Feb 2019

DC Katambi akutana na Harmonize, wafanya mazungumzo mazito


Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi amefanya mazungumzo na msanii maarufu wa Bongo Fleva kutoka WCB Harmonize aliyemtembelea ofisini kwake.

Katika mazungumzo hayo DC Katambi licha ya kumkaribisha msanii huyo pia alimueleza fursa za uwekezaji zinazopatikana jijini humo na kumtaka kuwa Balozi wa kuielezea Dodoma vizuri ili kuwavutia wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi waweze kuwekeza ndani ya Mkoa huo.

Kwa upande wa Harmonize aliahidi kuitangaza Dodoma kila mahali atakapopita, pia alimkabidhi DC Katambi t-shirt yenye nembo ya ‘Mixtape’ yake mpya inayoitwa Afro Bongo yenye nyimbo tano itakayotoka Februari 18 mwaka huu akiwa ameshirikiana na wasanii wakubwa barani Afrika akiwemo Diamond Platnumz, Burna Boy na Yemi Alade (Wote kutoka Nigeria).

Wakati huo huo DC Katambi amekutana na kufanya mazungumzo na waandaaji wa filamu iitwayo Salome kutoka kampuni ya Steps Entertainment Ltd inayozungumzia ugonjwa wa Fistula.



Katika mazungumzo hayo waandaaji hao walimualika DC Katambi kushiriki katika uzinduzi wa filamu hiyo utakaofanyika Machi 29, mwaka huu jijini Dodoma huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan.

"Niwapongeze nyinyi wasanii kwa kuamua kuandaa filamu hii kwa lengo la kuelimisha, hii ni kuonesha jinsi gani mlivyo na lengo zuri la kuisapoti Serikali yenu inayoongozwa na Rais wetu Dk John Magufuli, na mimi naahidi kuwaunga mkono ili kufanikisha jambo hili," DC Katambi.