Trump kuiondoa Marekani katika Mkataba wa Silaha wa UN - MULO ENTERTAINER

Latest

27 Apr 2019

Trump kuiondoa Marekani katika Mkataba wa Silaha wa UN

Katika mwendelezo wa sera zake kuu za kujitoa kwenye mikataba na makubaliano ya kimataifa, Rais Donald Trump wa Marekani ametangaza azma ya kuiondoa nchi hiyo katika Mkataba wa Uuzaji Silaha wa Umoja wa Mataifa (ATT).

Trump alitoa tangazo hilo jana Ijumaa, wakati akiwahutuhubiwa wanachama wa Chama wa Wamiliki wa Bunduki nchini humo NRA, ambacho kilifadhili asilimia kubwa ya kampeni zake katika uchaguzi wa mwaka 2016.

Trump amesema, "Tutachukua sahihi yetu. Hatuwezi kusalimisha uhuru wa kujitawala Marekani kwa mtu yeyote."

Mkataba huo wa ATT wa kudhibiti biashara ya silaha duniani ulisainiwa na mtangulizi wa Trump, Barack Obama mwaka 2013, lakini ukapingwa vikali na Chama wa Wamiliki wa Silaha NRA na makundi mengine ya kihafidhina nchini humo.

Tarehe 20 Oktoba 2018, Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kuwa nchi yake itajiondoa pia kwenye mkataba wa silaha za nyuklia za masafa ya kati (INF).

Chunguzi za kila mwaka za  taasisi ya Stockholm International Peace Research Institute (SIPRI) zimekuwa zikibaini kuwa, Marekani ndiye muuzaji mkubwa zaidi wa silaha duniani, huku Saudi Arabia ikishika nafasi ya kwanza kwa kununua silaha katika eneo la Mashariki ya Kati.

Trump ameiondoa Marekani kwenye mikataba mingi ya kimataifa tangu ashike hatamu za uongozi, kama vile makubaliano ya nyuklia ya Iran (JCPOA), Makubaliano ya Tabianchi ya Paris, pamoja na mikataba mingine mingi.