Serikali Yaajiri Walimu Wapya 4,549 - MULO ENTERTAINER

Latest

27 Apr 2019

Serikali Yaajiri Walimu Wapya 4,549

Serikali kupitia Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(OR-TAMISEMI) imepata kibali Cha kuajiri jumla ya walimu 4549 Kati ya 91108 walio tuma maombi yao.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo 27 Mei 2019 Magogoni, Dar es Salaam, Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI, Seleman Jafo amesema kuwa Rais Dk.John Pombe Magufuli katika kuhakikisha Serikali inawahudumia vizuri wananchi ameamua kufungua dirisha la ajira kwa walimu.

Jafo alisema jumla ya waombaji 91108 waliojitokeza na kutuma maombi yao katika nafasi mbalimbali na kati ya hayo 43770 sawa na asilimia 48.04 yalikuwa na viambatanisho vyote vilivyohitajika.

Hata hivyo alieleza kuwa maombi 47338 sawa na asilimia 51.96 hayakuwa na vigezo ikiwa ni pamoja na kukosa viambatanisho muhimu vilivyohitajika.

" Kutokana na mahitaji makubwa kwa walimu katika shule za msingi na sekondari kwa masomo ya sayansi, Tamisemi imefanya uchambuzi na kutoa vipaumbele katika ajira za walimu daraja la tatu (A) cheti kwa ajili ya kufundisha shule za msingi.

"Walimu daraja tatu (B) stashahada wa masomo ya sayansi kwa ajili ya kufundisha shule za sekondari( kidato cha kwanza hadi nne); na walimu daraja la tatu (C)shahada, wa masomo ya sayansi kwa ajili ya kufundisha kwa kidato cha tano na sita," alisema Jafo.

Pia walimu daraja la tatu (C) shahada, wa masomo ya elimu maalum , biashara, uchumi, kilimo na maarifa ya nyumbani kwa ajili ya kufundisha shule ya sekondari.

" Mchakato wa kupitia maombi ulijumuisha uhakiki wa uhalali wa vyeti vya elimu ya taaluma vya waombaji na ukamilishaji wa nyaraka zilizohitajika," alisema Jafo.

Aidha Jafo alieleza kuwa waombaji wa masomo ya sayansi na sanaa waliotimiza vigezo na hawakufanikiwa kupata nafasi kwa kipindi hiki, maombi yao yamechambuliwa na yamehifadhiwa kwenye kanzidata ya Tamisemi.

Alisema kwa walimu hao pindi fursa za ajira zitakapojitokeza utaratibu wa ajira utatolewa dhidi yao.

"Jumla ya walimu 4549 wamepangiwa moja kwa moja kufundisha shule zilizo na uhitaji wa walimu ambapo 3059 shule ya msingi na 1490 kwa sekondari," alisema.

Jafo alisema kuwa walimu wote waliopata ajira wanatakiwa kuripoti kwa wakurugenzi wa Halmashauri zenye shule walizopangiwa kwa ajili ya kuhakikisha vyeti vyao na kujaza mikataba ya ajira Kisha kuripoti kwenye vituo vyao kuanzia Mei 7, mwaka huu.

Jafo alisema walimu wapya ambao hawataripoti katika vituo vyao ifikapo Mei 21, 2019 nafasi zao zitajazwa moja kwa moja na walimu walio na sifa ambao hawakupangiwa bila kuwataarifu.

" Wakurigenzi wa Halmashauri wasikubali kubadilisha vituo vya kazi vya walimu bila kibali Cha katibu mkuu wa OR-TAMISEMI. Walimu Hawa tumewapangia kulingana na mahitaji ya sehemu husika.

Hata hivyo alisema kwa mwajiriwa atakayeripoti nakuchukua posho ya kujikimu Kisha akaondoka katika kituo chake cha kazi alichopangiwa atachukuliwa hatua kali za kisheria.