Kinana Ampiga Stop Mwigulu Nchemba, Amtaka Asitishe Ziara Zake Zote za Mikoani - MULO ENTERTAINER

Latest

20 Jan 2015

Kinana Ampiga Stop Mwigulu Nchemba, Amtaka Asitishe Ziara Zake Zote za Mikoani

Mwigulu Nchemba Ziarani
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana anadaiwa kuwa amepiga marufuku ziara zinazofanywa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Mwigulu Nchemba.

Mwigulu ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha na Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi mkoani Singida amekuwa akifanya ziara za kuzunguka wilaya na mikoa mbalimbali kwa kutumia usafiri wa helikopta.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti kwa masharti ya majina yao kutoandikwa gazetini, maswahiba wake walidai kuwa wameona barua ambayo Mwigulu ameandikiwa na Kinana ya kumtaka kuacha kufanya ziara hizo mara moja.

Kwa mujibu wa marafiki hao wa Mwigulu ni kwamba barua hiyo ya Kinana kwa sehemu kubwa inaeleza namna ambavyo amekuwa akifanya ziara nyingi katika mikoa na wilaya bila ushirikishwaji kamili wa makao makuu, mikoa na wilaya hasa kamati za siasa.

“Nimeona ile barua ambayo Mwigulu amenitumiwa, kuna sehemu inaeleza wazi kuwa kwa kauli na matendo yake ameonesha kujiandaa kugombea nafasi ya wewe, pia umeshaonesha kwa kauli na matendo yake kujiandaa kugombea nafasi ya urais kupitia CCM.

“Na kwamba ziara anazofanya mikoani na wilayani zinamuelekeo wa kampeni, jambo ambalo ni kinyume cha maadili ya chama,” alisema mmoja wa rafiki wa karibu wa Mwigulu wakati akizungumzia barua hiyo.

Alidai pamoja na maelezo mengine yaliyomo kwenye barua hiyo ya Kinana kwa Mwigulu kuna eneo ambalo anaagizwa kusitisha ziara zote na iwapo atataka kufanya ziara yoyote ya kichama itabidi apate kibali chake na kutakiwa kutekeleza maagizo hayo mara moja.

Kwa mujibu wa marafiki hao wa Mwigulu ni kwamba sababu za kufahamu kama kuna barua ya onyo amepewa ni kutokana na kulalamikia kupewa barua hiyo. Hata hivyo, hawakuwa tayari kueleza kama amekubali kusitisha ziara zake au la.

Wakati kukiwa na taarifa hizo za Kinana kumpiga ‘stop’ Mwigulu kufanya ziara hizo baadhi ya wadau wa siasa wamekuwa wakihoji wapi anakopata fedha kwa ajili ya kukodi helikopta anayotumia kwenye ziara zake kwa kuzunguka mikoa mbalimbali.

Pamoja na hayo, Mwigulu ameendelea na ziara zake katika maeneo mbalimbali ambapo juzi alikuwa mkoani Tanga kabla ya kwenda Morogoro.

Hata hivyo, Mwigulu hakuweza kuelezea kama amepewa barua na Kinana inayomtaka asitishe ziara zake.