Michezoni: Kocha wa Yanga FC adai Mrisho Ngassa Ameshuka kiwango katika mpira - MULO ENTERTAINER

Latest

8 Jan 2015

Michezoni: Kocha wa Yanga FC adai Mrisho Ngassa Ameshuka kiwango katika mpira



Kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm amesema winga Mrisho Ngasa ameshuka kiwango lakini atarejea katika makali yake muda si mrefu kwa sababu winga huyo ni "mchezaji mwenye akili nyingi".

Akizungumza na NIPASHE jana visiwani hapa jana, Pluijm alisema tangu arejee nchini Desemba kuinoa timu hiyo ya Jangwani baada ya kutimuliwa kwa Mbrazil Marcio Maximo, amekuwa akimwacha benchi mchezaji huyo wa zamani wa Kagera Sugar, Toto African, Simba na Azam FC kutokana na kushuka kiwango.

"Ni kweli Ngasa ameshuka kiwango ndiyo maana akacheza dakika saba tu katika mechi yetu dhidi ya Azam na hapa Zanzibar anacheza dakika chache pia. Azam ni timu nzuri ambayo unapaswa kuwa na mbinu za uhakika kabla ya kuingia uwanjani kuikabili.

"Ninaamini muda si mrefu atarejea katika kiwango chake. Ngasa ni mchezaji mwenye akili nyingi," alisema raia huyo wa Uholanzi.

Akiwa chini ya Pluijm na msaidizi wake Boniface Mkwasa, Ngasa alifunga mabao 13 na kutoa pasi za mwisho 17 katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu uliopita akiibuka mfungaji bora wa Yanga huku akifunga mabao sita na kutwaa tuzo ya mfungaji bora wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika.

Hata hivyo, msimu huu haukuanza vyema kwa nyota huyo ambaye kwa miaka kadhaa amekuwa akiibeba timu ya taifa akiifungia magoli 22 katika mechi 82 alizoichezea.