Itakumbukwa kuwa serikali ilifanya kampeni kubwa juu ya suala hili mwaka jana 2014. Na ikasema imejiandaa vya kutosha kuwaendeleza vijana hao wa masomo ya sayansi ili wamalizapo diploma ya “chap chap” warudi kwenye shule zetu kuondoa tatizo la ukosefu na upungufu wa walimu wa sayansi.
Vijana hao walidahiliwa pale Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kwa ajili ya programu hiyo lakini serikali haikuwa imejipanga kuwapa fedha za mahitaji muhimu kama ilivyohitajika. Taarifa kutoka UDOM zinaonesha kuwa, vijana hao wametangatanga na kuomba pesa za kula na kujikimu kutoka kwa wale “wakubwa zao” wanaosoma Digrii hadi imekuwa kero.
Unakuta kisichana cha miaka 17 au 16 kinasoma programu hii na hakijapewa pesa za vitabu, chakula na malazi. Kinazunguka kuwaomba wakaka wa digrii ili kiishi, nani kakipeleka kitoto hiki Dodoma? Baada ya vijana hao wanaotokea mikoa mbalimbali ya Tanzania kutaabika bila kupata msaada huku hawana pesa kwa muda mrefu, waliamua kuongozana kwenda kwa Waziri Mkuu na ama Mawaziri na viongozi wengine wa serikali ili suala lao litatuliwe. Wamekutana na ukatili wa kutosha kutoka kwa polisi, wengine wamevunjika na kuumia vibaya.
Mimi ambaye nimepitia misukosuko zaidi ya hiyo wakati naongoza UDSM na TAHLISO, nachoweza kusema ni kuwa vijana wa sasa na wazee wetu wa sasa, hii ndiyo hali halisi ya nchi yetu. Tuna serikali isiyo na mipango na isiyo na haja ya kupanga na kutekeleza chochote “unresponsible government”.
Iweje tupange kusomesha vijana kwa programu za dharura huku hatuna fedha za kuendesha program hiyo na hasa kutosheleza mahitaji ya gharama za maisha ya wahusika? Ni hivi karibuni tu Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu imetangaza kwamba imeshindwa kuwapa mikopo wanafunzi zaidi ya 20,000 kwa mwaka huu peke yake.
Nikukumbusheni pia kwamba, bunge la bajeti lililokamilisha kazi yake mwezi Juni 2014 tulijionea ripoti za aibu zikionesha kuwa kuna wizara nyingi tu ziliishia kupata 40% - 50% ya bajeti iliyopangwa. Haya yote ni dalili tosha kuwa tunaishi kwenye “taifa linaloangamia” (a failed state). Kwamba hatuna uwezo wa kupanga na kutekeleza mipango yetu.
Kwamba hatuna kipaumbele kwa yale tunayoyafanya. Watoto wa watu tumewadanganya, wameacha kwenda kidato cha tano na sita kwa nia njema ya kulisaidia taifa lao kutokana na vipaji na elimu yao, badala ya kuwalipa neema na mipango thabiti tunawalipa ubabaishaji, ukatili, nia ovu na jeuri. Vijana hawa wanaoteseka leo kwa ajili ya haki zao wanapata mafunzo makubwa sana.
Idadi ya vijana watakaoendelea kuichukia CCM inaongezeka kama mchanga wa baharini maana “Colonialism planted the seeds of its own destruction” – Hakika, hata CCM inapanda mbegu ya kujimaliza wenyewe. Poleni sana wadogo zetu, poleni sana wana UDOM