NDOA iliyodumu kwa miaka miwili na nusu kati ya mwigizaji wa filamu Jacqueline Pentzel na Gadna Dibibi imevunjika, Ijumaa lina mkanda kamili.
Kwa mujibu wa chanzo makini, wawili hao waliachana baada ya kutuhumiana kutoka nje ya ndoa yao, jambo ambalo baada ya kuvumiliana kwa muda mrefu, hatimaye wameamua kubwaga manyanga.
Inadaiwa kwamba kwa zaidi ya miezi miwili iliyopita, mume alikuwa ameshahama nyumbani kwao Mbezi kwa Msuguri walikokuwa wakiishi na kuhamia Ilala na Kijitonyama kwa ndugu zake.Baada ya taarifa hizo, gazeti hili liliwasiliana na Gadna ambaye alisema:
“Ni kweli tuna wiki kama mbili tatu hatupo pamoja, kuna mambo tumeshindwana, na kweli nimemwandikia talaka na kila mmoja sasa anaishi kimpango wake,” alisema Gadna.
Naye Jack alipopatikana alikiri kutokea kwa jambo hilo na kwamba talaka yake imeshaandikwa, isipokuwa bado hajaenda kuifuata Kijitonyama kwa ndugu wa aliyekuwa mumewe.Licha ya kudaiwa kuwa ishu ya uchepukaji ndiyo sababu, hakuna aliyekuwa tayari kufunguka juu ya hilo.