Rais Kikwete Afichua SIRI Kipigo cha Lipumba.....Asema sheria za nchi lazima Zifuatwe - MULO ENTERTAINER

Latest

4 Feb 2015

Rais Kikwete Afichua SIRI Kipigo cha Lipumba.....Asema sheria za nchi lazima Zifuatwe

SIKU chache baada ya Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba na wafuasi wake kupigwa na polisi, Rais Jakaya Kikwete amesema tukio hilo limetokea kwa sababu 
nchi inaongozwa kwa sheria na atakayekiuka atakumbana na mkono wa sheria.

Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jana Ikulu jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufanya mazungumzo ya faragha na mgeni wake, Rais wa Ujerumani, Joachim Gauck, ambaye yuko nchini kwa ziara ya siku tano.

Kabla ya Rais Kikwete kutoa kauli hiyo, Rais Gauck aliimwagia sifa Tanzania kutokana na namna inavyofuata utawala wa sheria, uhuru wa vyombo vya habari na kulinda haki za binadamu.

Baada ya viongozi hao kuzungumza mbele ya waandishi wa habari juu ya ziara hiyo, waandishi walipewa fursa ya kuuliza maswali na ndipo mmoja wa wanahabari kutoka Ujerumani, alipotaka kauli ya Rais Kikwete na Rais Gauck, juu ya msingi wa uhuru wa vyombo vya habari na haki za binadamu nchini, wakati hivi karibuni gazeti la The East African lilifungiwa na wanachama wa CUF kupigwa na polisi walipotaka kuandamana.

Akijibu swali hilo, Rais Kikwete alisema: “Tuna sheria zinazoongoza mambo hayo, huwezi kuamka tu ukaamua kuandamana, tuna taratibu zetu za vyama vya siasa kukusanyika, wala hatubani haki na uhuru wa wapinzani, ukivunja sheria hiyo utawajibishwa.

“Na hapa wapinzani ndio wanafanya mikutano mingi kuliko chama tawala, ikitokea hawajafuata taratibu, hatuwezi kuwaacha waendelee kuvunja sheria,” alisema Rais Kikwete.