Ushauri kwa Waislamu Wote Tanzania, Hasa Walio Mtandaoni - MULO ENTERTAINER

Latest

5 Feb 2015

Ushauri kwa Waislamu Wote Tanzania, Hasa Walio Mtandaoni

Nimefikiria muda mrefu kuhusu sakata hili la kufa na kupona la mahakama ya kadhi. Ni wazi kuwa mahakama ni muhimu katika jamii. Lakini pamoja na umuhimu wake, nadhani tukikaa chini na kutafakari, kuna mengi ya umuhimu zaidi. Jambo la kwanza .......
kwa Nchi kama Tanzania ambayo kwaajili ya uongozi mbovu wa waliokuwa madarakani kwa nyakati tofauti lingepaswa kupewa kipaumbele ni Elimu. Ona jinsi Elimu inavyochezeshwa gwaride, hadi tumefikia hatua ya kuweka div. 5, ili kuficha waliofeli.

Nirudi kwenye mada,
Nasema ushauri kwa waislamu kuwa waongeze nguvu kwenye elimu dunia. Waongeze shule zinazoendeshwa na taasisi za kiislamu, zenye ubora. Waongeze vyuo vikuu vinavyoendeshwa na taasisi za kiislamu, wakitaka wawapokee waislamu tu haidhuru, lakini ni bora wakawapokea wote kama zifanyazo taasisi za kikristu. Elimu bora Tanzania inahitajika. Na Elimu bora Tanzania haiwezi kutolewa na Serikali tu. Ona madhehebu ya kikristo walivyoweka kipaumbele katika elimu. Hesabu tu vyuo vikuu vinavyoendeshwa na madhehebu ya kikristo. Hesabu shule za sekondari zenye ubora wa hali ya juu zinazoendeshwa na taasisi za kikristo. Sijui taasisi za kiislam zinaendesha vyuo vikuu vingapi, lakini nafahamu walau moja ile ya Morogoro, iliyokuwa chuo cha Tanesco, ambayo walipewa na serikali ili kuwatuliza.

Tazama kwenye afya, ona ni vituo vingapi vya afya, hospitali, hadi hospitali za rufaa zinazoendeshwa na taasisi za dini? Nafahamu walau hospitali ya rufaa ya KCMC na Bugando zinaendeshwa na taasisi za kikristo. Hospitali za kawaida ni nyingi. Zinazoendeshwa na taasisi za kiislamu sizifahamu, zinaweza kuwa nyingi kuliko hizo, au la. Kwenye suala la afya ndipo pa kutumia nguvu nyingi. Huko ndipo pa kuwa na hitaji la kuweka kambi Bungeni kama kutakuwa na haja.

Nadhani sio vizuri kusubiri siku zote kubebwa na serikali. Kila madhehebu wana sheria zao, sheria zao ambazo hazipaswi kwenda kinyume na sheria za Nchi. Sioni sababu ya kutumia nguvu kubwa kudai mahakama badala ya kuwekeza kwenye mambo ya maandeleo kama elimu, afya, nk. Kwanini tunadhani maisha yetu lazima kupelekana mahakamani?

Ndiyo maana nasema natoa ushauri kwa waislamu hasa waJF maana ndo watakaosoma ushauri huu, Waislamu wawekeze nguvu nyingi kwenye mambo ya maendeleo zaidi kuliko mahakama. Wawekeze kwenye elimu na afya. Achaneni mambo ya mahakama. Mahakama ya nchi inaweza kumaliza yote, ikiwa kutakuwa na haja. Lakini kwa mtu optimistic hawezi kutumia nguvu nyingi kwenye hilo.

Sio haki kwa wabunge: wawakilishi wa wananchi kupoteza muda kujadili kuwa waislamu wawe na mahakama ya kadhi au la. Ni wazi watajadili, hasa wakati huu tunapokaribia uchaguzi. Ili kila mchangiaji aonekane anawajali waislamu, ataunga mkono mahakama ya kadhi, watafanya funika kombe mwanaharamu apite. Ili tu waislamu wa jimbo lake wasimtose, ili tu waislamu wasikikatae chama chake. Lakini nasema tena sio haki wabunge wapoteze muda katika jambo hili ambalo sio kipaumbele cha taifa. Sio haki lakini litajadiliwa kwaajili wa woga wa kupoteza kura.

Mniwie radhi, kama kuna moja hatapendezwa na ushauri wangu. Ukweli utabaki kuwa kuwekeza kwenye elimu, hasa elimu dunia na afya ni bora kuliko kuwekeza kwenye mahakama.