Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetahadharishwa kisifanye mzaha na uteuzi wa mgombea wa nafasi ya urais kupitia chama hicho, kwani kisipoteua mtu makini na mchapa kazi anayekubalika na jamii, mgombea atakayesimamishwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), atashinda kirahisi urais uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu.
Akizungumza kwenye mazishi ya kada maarufu wa CCM wilayani Kahama, Emmanuel Chupa, Diwani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kata ya Nyasubi, Leonard Mayala, alisema ana amini chama hicho kitakosea iwapo hakitampitisha Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa kuwania urais, ambaye anaonekana ana nguvu ndani ya chama hicho na ataisumbua Ukawa katika uchaguzi mkuu ujao.
Alisema kwa hali ya kisiasa inavyoonekana nchini kwa sasa, ni wazi Watanzania wanahitaji Rais ajaye awe mwenye uwezo mkubwa wa kufanya kazi na uzoefu katika masuala ya uongozi na kiutawala na si kuchagua kiongozi wa kwenda kujifunza kufanya kazi Ikulu.
Hata hivyo, alisema imani yake ni CCM itateleza katika uteuzi wake na kuteua mgombea asiyekubalika kwa Watanzania wengi, hivyo kutoa nafasi kwa Ukawa kuongoza nchi.
“Licha ya mimi kutoka kambi ya upinzani, lakini na amini Lowassa akiteuliwa na CCM atasukuma kasi ya maendeleo na kuongeza pato la mtu mmoja mmoja na uchumi wa taifa kwa ujumla,” alisema.