Watu 18 walifariki papo hapo kwa kuteketea kwa moto na wengine 11 kujeruhiwa vibaya kutokana na basi walilokuwa wakisafiria kugongana na lori aina ya Mitsubishi Fuso, katika kijiji cha Msimba tarafa ya Mikumi, barabara kuu ya Morogoro – Mbeya hapo jana.
Ajali hiyo imehusisha basi la Kampuni ya Nganga linalofanya safari zake kutoka Wilaya ya Kilombero kuelekea mkoani Mbeya na kugongana na lori hilo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonald Paulo alisema ajali hiyo ilitokea jana saa mbili asubuhi katika eneo hilo huku likihusisha basi aina ya Scania lenye namba za usajili T373 DAH na Fuso lenye namba za usajili T164 BKG.
Alisema chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa basi la Nganga ambaye alikuwa katika mwendo kasi na kulipita gari lililokuwa mbele yake bila ya tahadhari na kukutana na lori hilo na kisha kugongana nalo katika eneo hilo.
Alisema baada ya magari hayo kugongana, ndani ya buti ya basi kulikuwa kumepakiwa pikipiki ambayo ilikuwa na mafuta na baada ya kutokea ajali hiyo kulitokea mlipuko wa moto na kusababisha basi hilo pamoja na lori kuwaka moto.
Kamanda huyo alisema kuwa kutokana na moto huo, baadhi ya abiria waliokuwepo katika basi hilo walishindwa kujiokoa na hivyo miili yao kuteketea kabisa na moto huo, wakiwemo madereva wote wa magari hayo.
Alisema majeruhi 11 wa ajali hiyo wamekimbizwa katika Hospitali ya Mtakatifu Kizito iliyopo tarafa ya hiyo Mikumi kupatiwa matibabu huku hali zao akieleza kuwa baadhi yao ni mbaya kutokana na kuungua vibaya kwa moto.
Kamanda huyo alisema miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika hospitali hiyo ambapo mpaka sasa haijatambulika majina yake, licha ya madereva wa magari yote kufa.
Hata hivyo, Kamanda huyo alishindwa kutaja majina ya majeruhi kutokana na baadhi yao kuendelea kupatiwa matibabu kwa ajili ya kuokoa maisha yao.
Naye Mganga wa Hospitali ya Mtakatifu Kizito iliyopo Mikumi, Dk Boniventure Buyagabuyaga, alithibitisha kupokea jumla ya miili ya marehemu 18 ambao walikuwa wameteketea vibaya kwa moto kutokana na ajali, ambapo alisema tayari imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhiwa maiti kwa ajili ya kusubiri utambuzi.
Alisema mpaka sasa majeruhi wanaotibiwa katika hospitali yake wamebaki saba, lakini hali zao bado ni mbaya kutokana na kuungua moto katika sehemu mbalimbali za miili yao.
Ajali hiyo imekuwa sawa na mwendelezo wa ajali za mabasi nchini, kwani Alhamisi iliyopita watu 12 walikufa katika ajali zilizotokea Tanga na Morogoro, huku wengine wanne waliokuwa wakisafiri kwa basi la Nyehunge wakiaga dunia usiku wa Jumamosi mkoani Dodoma.
Katika ajali iliyotokea mkoani Tanga, katika kijiji cha Mbweni Mkata, majira ya asubuhi, ilihusisha basi la Kampuni ya Ratco ya Tanga liligongana uso kwa uso na basi la kampuni ya Ngorika na gari dogo aina ya Toyota Passo na kusababisha vifo vya watu 10 papo hapo, akiwemo mmiliki wa gari dogo, Musa Lupatu aliyekuwa Mbunge wa zamani wa Korogwe Vijijini.
Katika tukio la Morogoro, watu wawili walikufa na wengine 48 kujeruhiwa katika ajali iliyosababishwa na basi la Happy Nation lililokuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Mbeya na kupata ajali eneo la Mikumi.
Aidha, Machi 12, mwaka huu mkoani Iringa, basi la Majinja Express lilikuwa likitokea Mbeya kwenda Dar es Salaam liligongana na lori na kisha likaangukiwa na kontena lililosababisha vifo vya watu 43.