Shirikisho la Soka Tanzania(TFF) limemteua Charles Boniface Mkwassa, kuwa kocha mpya wa Timu ya Taifa ya Soka ya Tanzania(Taifa Stars) - MULO ENTERTAINER

Latest

24 Jun 2015

Shirikisho la Soka Tanzania(TFF) limemteua Charles Boniface Mkwassa, kuwa kocha mpya wa Timu ya Taifa ya Soka ya Tanzania(Taifa Stars)

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania - TFF, Jamal Malinzi leo ameagana rasmi na aliyekua kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager, mholanzi Mart Nooij.

Akiongea na waandishi wa habari leo katika hoteli ya Tansoma, Malinzi amesema wameamua kuagana nae mbele ya vyombo ya habari kama iliyofanyika pia wakati wa utambulisho wake wakati wa kuanza kazi.

“Mpira wa miguu unachangamoto nyingi, watanzania tunasafari ndefu katika mafanikio ndio maana TFF imeanza kuwekeza katika soka la vijana, sababu ndio msingi wa kuwa na timu bora ya Taifa” alisema Malinzi.

Duniani kote chimbuko la timu bora ni soka la vijana na watoto, tukiwa na vijana wengi walioanza kucheza mpira katika umri mdogo wanapofikia umri wa kuchezea timu ya Taifa tutakua na kikosi bora.

Nchi za wenzetu inapofikia kocha kuita wachezaji wa timu ya Taifa anakuwa na wigo mpana, kwetu sisi wachezaji wanocheza soka nje ya nchi wanahesabika, hivyo ni lazima tuanze kuwekeza kwenye soka la vijana.

TFF ilishaanza mkakati huo ndio maana kuna timu za U13, U15 ambazo zitakua zikiingia kambini na kucheza michezo ya kirafiki ndani ya nje kwa lengo la kupata uzoefu kabla ya kushiriki kuwania kufuzu kwa fainali za vijana mwaka 2016.

Kikosi cha U15 kinatarajiwa kufanya ziara mwezi Disemba mwaka huu katika nchi za Malawi, Zambia, Zimbambwe, Botswana na Afrika Kusini, kisha mwakani mwezi April 2016 kitaenda Rwanda, Burundi, Uganda na Kenya kucheza michezo ya kirafiki.

Naye Mart Nooij aliyekua kocha wa Taifa Stars, akiongea na waaandishi wa habari alisema anawashukuru watanzania wote, serikali, wadau wa mpira wa miguu nchini na TFF kwa sapoti waliyompatia wakati akiwa kocha mkuu wa timu ya Taifa.

Nooij alisema alifurahia maisha yake akiwa Tanzania kwa kipindi chote alichokua akifundisha timu ya Taifa, lakini kwa sababu imefikia mwisho wa ajira yake hana jinsi anaondoka, lakini ataendelea kuikumbuka Tanzania na watanzania wote kila siku kwa ukarimu wao.

Wakati huo huo Rais wa TFF. Jamal Malinzi amemtangaza Charles Mkwasa kuwa kocha mpya wa Taifa Stars akisaidiwa na kocha Hemed Morocco, Mkwasa ambaye ni kocha wa Yanga na Morocco kocha wa Mafunzo watafanya kazi kwa kipindi cha miezi mitatu ambayo timu ya taifa itakua na michezo ya kuwania kufuzu kwa CHAN na AFCON.

Malinzi amesema uteuzi wa makocha hao wazawa umezingatia vigezo vya makocha wa timu ya Taifa kuwa na leseni A ya ukocha kutoka CAF au zinazofanana kutoka mashiriksho mengine duniani wanaozifanyia kazi, jambo ambalo makocha hao wazawa wamekizi.

Kocha Mkwasa atakua akipewa hudumu zote na masilahi (zikiwemo posho) alizokuwa anapewa kocha aliyeondoka, pia amepewa nafasi ya kuchagua benchi lake la ufundi la kufanya nalo kazi, hivyo nawaomba wadau wa mpira wa miguu na watanzania kwa ujumla tuwape sapoti makocha hao wazawa” aliongeza Malinzi”

Aidha Kamati ya utendaji ya TFF Iimemteua Alhaj Ahmed Mgoyi kuwa mratibu wa timu ya Taifa, lengo la uteuzi huo wa Mgoyi ni kuwa kiunganishi kati ya kamati ya Utendaji na timu ya Taifa.

U15 Yaingia  Kambini
Timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 15 ya Tanzania, imeingia kambini jana na kuanza mazoezi leo katika uwanja wa Karume kujiandaa na mchezo wa kirafiki dhidi ya kombaini U15 ya mkoa wa Mbeya siku ya jumapili.

Kikosi hicho kilicho chini ya makocha Bakari Shime na Peter Manyika kitacheza mchezo huo kwa lengo la waalimu kupatawa fursa ya kuwaona vijana hao na kuwaongeza wengine watakaoneka katika kikosi hicho.

U15 ni mpango wa TFF kuandaa kikosi kizuri chenye ubora kuelekea kuwania kufuzu ka fainali za vijana Afrika mwaka 2017 zitakazofanyika nchini Madagascar, ambapo vijana hao watakua na umri wa miaka 16 kufikia mwakani wakati michezo ya kuwania kufuzu itakaponza mwezi Julai, 2016.

NB: Kesho siku ya jumatano kocha mpya wa Taifa Stars, Charles Mkwasa na msaidizi wake Hemed Moroco wataongea na waandishi wa habari saa 5:30 asubuhi katika ukumbi wa mikutano wa TFF uliopo Karume.

Waandishi wote wa habari mnaombwa kuhudhuria bila kukosa.

Imetolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania