Hatimaye mke mdogo wa Dk. Willibrod Slaa, Josephine Mushumbusi, ameibuka na kujibu baadhi ya hoja ambazo zimekuwa zikielekezwa kwake yeye binafsi na kwa mume wake na zaidi akisema yote yanayosemwa dhidi yao hayako katika fikra zao kwani kwa sasa baada ya kuachana na siasa wanajipanga kuelekea upande mwingine wa kuwa wawekezaji.
Akizungumza na gazeti la mtanzania jana, Mushumbusi aliitaja mipango yao hiyo kuwa ni pamoja na kujenga shule na hospitali.
Mushumbusi ametoa kauli hiyo wakati ambapo gharama zinazokadiriwa kufikia shilingi milioni 50 alizozitumia mume wake katika mkutano wake na waandishi wa habari mapema wiki hii zikizua mjadala mpana wa alikopata fedha hizo zote.
Pamoja na hilo, Mushumbusi ambaye anatajwa kuwa katikati ya mpango wa kumrubuni mume wake licha ya kupuuza hoja kama hizo alipoulizwa walikopata fedha za kutekeleza miradi mikubwa kama hiyo alisema zimetoka kwa watu aliodai kuwa ni marafiki zao na kiasi kingine ni asilimia 20 ya vipato vyao ambavyo walikuwa wakiviweka kwa muda mrefu.
Mushumbusi ambaye tangu Dk. Slaa azungumze na waandishi wa habari Jumanne wiki hii hajawahi kuzungumza lolote, alianza kujibu yale yaliyozungumzwa na mke mwenzake ambaye ni mke wa ndoa wa Dk Slaa aitwae Rose Kamili ambaye juzi alizungumza na vyombo vya habari na kumtupia tuhuma nzito yeye (Mushumbusi) na mume wake huyo wa zamani.
Rose alikaririwa na vyombo vya habari akimtuhumu mumewe kuwa ni muongo na anapelekeshwa na mwanamke anayeishi naye kwa sasa ambaye ni Mushumbusi.
Akijibu shutuma hizo, Mushumbusi alisema yeye ni zaidi ya siasa rahisi zinazoenezwa dhidi yake.
Alimpuuza Rose kwa kusema kuwa ameamua kuchanganya matatizo binafsi ya familia na propaganda za kisiasa, hivyo jambo hilo liko mbali na uwezo wa fikra na mipango yake kwa sasa.
Mushumbusi alisema yeye si mwanasiasa kwani ana mambo mengi anayoyafanya mbali na siasa hivyo shutuma alizotoa Rose kwa Dk. Slaa zingefaa pia kama angewaeleza Watanzania sababu za kuachwa kwake.
“I’m above with that cheap politics, you know? (Unajua niko juu ya siasa hizo rahisi?), I’m activist, I can’t deal with them and I have a lot of things to do out of politics by the way, I’m not a politician as I told you (mimi ni mwanaharakati, siwezi kushughulika nao na nina mambo mengi ya kufanya nje ya siasa, hata hivyo mimi sio mwanasiasa kama nilivyokueleza),” alisema Mushumbusi.
Mushumbusi alifafanua kuwa hivi sasa yuko mbali na mambo ya siasa na anaangalia mbele kulisaidia taifa katika nyanja za elimu, afya na uchumi.
Alisema mipango yao kwa sasa ni kujenga shule, hospitali pamoja na kuwasaidia kina mama katika masuala ya ujasiriamali.
Alisema tayari mipango yao hiyo mipya ilikwishapangwa kwa kushirikiana na Dk. Slaa.
Alisema mbali na fedha za marafiki yeye ni mfanyabiashara wa nafaka na kwa muda mrefu pamoja na mumewe wamekuwa wakiweka akiba.
Hata hivyo, wakati Mushumbusi akisema kuwa anafanya biashara ya nafaka, gazeti moja la kila siku (Si MTANZANIA) liliwahi kumkariri hivi karibuni akidai kuwa kwa sasa anafanya biashara ya mkaa.
“Brother I’m not there as they think, I’m a focused woman (Kaka sipo hapo kama wanavyofikiri, mimi ni mwanamke makini), nina mambo mengi ya kulifanyia taifa langu, nashangaa hata hiyo hoja ya kutelekeza watoto, waulizeni hao watoto kama hawapajui kwangu, huyo kijana wa kiume kila mara anakuja kwangu hata wadogo zake wanamfahamu vyema, eti wanasema Dk. Slaa kawatelekeza wanataka awafanyie nini na wakati watoto wote hao ni above eighteen (zaidi ya miaka 18) na tayari wamezaa kila mmoja, hoja nyingine you must think big (kufikiri zaidi),” alisema Mushumbusi.
Kuhusishwa na Kinana, Lukuvi
Akijibu madai ya kutuhumiwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, William Lukuvi ili kumpa maelekezo mumewe juu ya nini afanye baada ya kujiengua Chadema, Mushumbusi alikana madai hayo kwa kusema kuwa hana mawasiliano yoyote na watu hao.
Akijibu madai ya kutuhumiwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, William Lukuvi ili kumpa maelekezo mumewe juu ya nini afanye baada ya kujiengua Chadema, Mushumbusi alikana madai hayo kwa kusema kuwa hana mawasiliano yoyote na watu hao.
“Sina mawasiliano na Kinana wala Lukuvi kwanza ni watu ambao sijawahi kufikiria hata siku moja kama nitazungumza nao, kwanza simpendi huyo Kinana,” alisema Mushumbusi.
Dk. Mwakyembe na Dk. Slaa
Kuhusu kukutana na Dk. Mwakyembe katika moja ya vyumba vya Hoteli ya Serena akiwa yeye na mume wake, Mushumbusi alikana taarifa hizo.
Kuhusu kukutana na Dk. Mwakyembe katika moja ya vyumba vya Hoteli ya Serena akiwa yeye na mume wake, Mushumbusi alikana taarifa hizo.
Hata hivyo, gazeti la mtanzania linafahamu kuwa Mushumbusi alikuwepo katika moja ya vyumba vya hoteli hiyo ambavyo mume wake alivitumia kukutana na Mwakyembe saa chache kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari.
Pamoja na ukweli huo, Mushumbusi alisema hana mawasiliano na Mwakyembe ingawa alikiri mume wake kukutana naye ili kupata ufafanuzi wa baadhi ya hoja za sakata la Richmond.
“Dk alihitaji kupata ufafanuzi fulani wa hoja za Richmond, kumbuka ripoti ya Richmond iliandikwa kisheria zaidi hivyo alimuhitaji Dk. Mwakyembe kwa ajili ya kupewa ufafanuzi wa baadhi ya vipengele ndipo walipokutana saa chache kabla ya mkutano na wanahabari,” alisema.
Chanzo: Mtanzania