Mke wa Lowassa Mama Regina Lowassa |
Hali hiyo inatokana na mgombea mmoja wa ubunge wa jimbo hilo kupitia CUF, Martine Makondo na wafuasi wake, kuvamia uzinduzi wa kampeni za mgombea ubunge wa CHADEMA, Martine Magire ambapo mgeni alikuwa Mama Regina Lowassa (mke wa Edward Lowassa).
Mama Lowassa alishindwa kuzindua kampeni hizo kutokana na vurugu kubwa zilizotokea. Awali mkutano ulikuwa ufanyike kwenye Uwanja wa Michezo uliopo katika Sekondari ya Lagangabilili.
Dalili za vurugu zilianza kuonekana mapema baada ya wafuasi wa CHADEMA kudai kuwa, mgombea wa CUF alikuwa amekwenda kwenye mkutano huo na kundi la vijana ili kuvuruga mkutano.
Baada ya Mama Lowassa kuwasili eneo la mkutano akiwa na Naibu Katibu Mkuu Baraza la Wanawake wa CHADEMA Taifa (BAWACHA),Kunti Yusuph, mgombea wa CUF aliwasili eneo hilo akiwa amebebwa na wafuasi wake wakidai mgombea wao amehujumiwa na mgombeawa CHADEMA na kusababisha jina lake likatwe na Kamati Kuu.
Wafuasi wa CUF walimpandisha mgombea wao (Makondo), jukwaani ndipo vikaanza kutokea vijembe kati yao na wafuasi wa CHADEMA wakiimba, kupiga kelele za kuwataja wagombea wao.
Hali hiyo iliwashangaza viongozi wa CHADEMA na mgeni rasmi (Mama Lowassa) kwa dakika 15 ndipo walinzi wa chama hicho wakamwondoa eneo hilo wakihofia usalama wake katika mkutano huo.
Baada ya Mama Lowassa kuondolewa jukwaani, kupanda gari yake na kuondoka eneo la mkutano, Yusuph alianza kuwatuliza wafuasi wa vyama hivyo bila mafanikio akaamua kuwatuhumu wananchi, lakini wafuasi walimzomea wakitaka Makondo arudishwe.
"Tatizo tunafanya siasa kwa ushabiki na matokeo yake ndiyo haya, mimi sikuja kunadi mahindi kwenye mnada, nimekuja kumwombea kura mgombea urais wa UKAWA (Edward Lowassa), ubunge na udiwani mtajuana wenyewe Oktoba 25, mwaka huu," alisema.
Hata hivyo, Yusuph alishindwa kutuliza vurugu hizo na kulazimika kuondoka eneo hilo chini ya ulinzi wa vijana wa CHADEMA na kuwaacha viongozi wa mkoa, wilaya waendelee na mkutano lakini hata baada ya kuondoka, mkutano huo haukuendelea.
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Gemin Mushy, alisema askari wake walitumia busara kutomtoa mgombea wa CUF kutokana na mazingira kutokuruhusu kumkamata.
Chanzo cha mgogoro huo ni Makondo ambaye awali alikuwa CHADEMA, kutimkia CUF baada ya jina lake kukatwa ingawa alishinda kwenye kura za maoni na aliyeshinda nafasi ya pili Magire kupewa nafasi hiyo.