Kuna taarifa ya kutunga inasambazwa kwa njia za mawasiliano ya mitandao ya kijamii hususan Facebook na WhatsApp ikieneza habari za uongo kuhusu Mwenyekiti wa Chama Taifa, Freeman Mbowe na Mgombea Urais wa CHADEMA anayeungwa mkono na vyama vinavyounda UKAWA, Edward Lowassa.
1. Chama hakijatoa taarifa yoyote kuhusu kuwepo kwa safari ya Mwenyekiti wa Chama Taifa, Freeman Mbowe. Hatujatoa taarifa hiyo kwa sababu hakuna habari ya Mwenyekiti Mbowe kusafiri.
Mwenyekiti Mbowe amekuwa kwenye campaign trail (field) ya Mgombea Urais katika maeneo kadhaa kabla ya kuendelea na shughuli zingine za campaign trail nje ya field, ofisini kwake jijini Dar es Salaam ambazo anaendelea nazo hadi sasa na leo Jumamosi, Septemba 19, atakuwa na mkutano na waandishi wa habari.
Ukiangalia kwa makini pia, taarifa hiyo ambayo imeitwa ni Barua ya Wazi kwa Vyombo vya Habari, haiko katika mwonekano wa taarifa sahihi na rasmi za chama ambazo huwa zinatolewa na/kwa uratibu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Chama.
2. Mgombea Urais wa CHADEMA anayewakilisha pia vyama washirika wenza vinavyounda UKAWA (CUF, NCCR-Mageuzi na NLD) anaendelea na ziara za kampeni mikoani akiwafikia wananchi wa vijijini na mijini. Habari zingine tofauti na hizo ni mwendelezo wa wapinzani wetu yaani CCM kutaka kuhamisha mjadala wa uchaguzi wa MABADILIKO ili wapiga kura wajadili vitu vingine visivyokuwa muhimu kwenye wakati ambapo Watanzania wanajiandaa kuandika historia mpya katika nchi yao.
Kubadili mjadala ndiyo mbinu ambayo CCM wameamua kuitumia ili eti kuwachanganya wapiga kura ambao wamejikita kutaka kusikia UCHAGUZI wa MABADILIKO. Si mabadiliko ya sura ndani ya CCM ile ile, bali mabadiliko ya kiutawala na kimfumo, kwa kuiondoa CCM madarakani na kukabidhi dhamana ya uongozi wa serikali na nchi kwa vyama vinavyounda UKAWA.
Kujikita kujadili porojo na uzushi kwa sasa badala ya agenda za uchaguzi huu unaolenga Mabadiliko, ni kuisaidia CCM inayopoteza uhalali wa kisiasa kadri uchaguzi unavyokaribia ili hata uhalali wa kisheria ilionao sasa, ukahitimishwe hapo Oktoba 25, mwaka huu.
Hatutawaachia wapumue kwa sisi kuanza kujadili uongo wanaozusha. Wananchi wana matumaini makubwa na UKAWA. Wanaimba mabadiliko na Lowassa, Lowassa na Mabadiliko. Wanasubiri mabadiliko kutoka kwa CHADEMA, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.
Tunasimamia hapo kusonga mbele.
19 Sept 2015
New
mulo
Siasa