Rais Dr. Magufuli na Mhe. Majaliwa: Karata za CCM kisiasa, zitafanikiwa? - MULO ENTERTAINER

Latest

20 Nov 2015

Rais Dr. Magufuli na Mhe. Majaliwa: Karata za CCM kisiasa, zitafanikiwa?

Natazama kuteuliwa kugombea na baadaye kuchaguliwa kuwa Rais wa Tanzania kwa Dr. Magufuli kwa tiketi ya CCM kama karata muhimu iliyochangwa na kuchezwa na CCM katika uchaguzi uliopita. Iko wazi kuwa CHADEMA kama chama kikuu cha upinzani Tanzania, kilijijenga vya kutosha katika maeneo ya Kanda ya Ziwa yenye mikoa ya Mara, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Geita na Kagera. Kitendo cha kusimamishwa kwa Dr. Magufuli ni kitendo cha kutikisa ngome ya CHADEMA.

Dr. Magufuli ni mwenyeji wa kanda hiyo kwakuwa amezaliwa, kukua, kufanya kazi na kuwa Mbunge huko Chato mkoani Geita. CHADEMA iliachwa mkono na wananchi wa kanda ya ziwa si kwakuwa ilipoteza umaarufu. Iliachwa mkono kwakuwa tu wananchi wa kanda ya ziwa waliona mwaka huu ni 'zamu yao' kutoa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hususani kabila kubwa kuliko yote nchini-wasukuma.

Kuibuliwa kwa Dr.Magufuli ni karata ya kukata nguvu za upinzani-hasa CHADEMA katika Kanda ya Ziwa iliyoonja ladha ya operesheni mbalimbali za kichama katika kujenga na kuimarisha CHADEMA. Kama hiyo haitoshi, CCM imecheza karata nyingine leo kupitia kwa Rais Magufuli kumteua Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania. Kanda ya kusini inasemwa kama kanda iliyo nyuma kuliko zote kimaendeleo.

Pia kanda hiyo ina vuguvugu la gesi asilia lililopelekea wananchi wa huko kupunguza kuipenda na kuishabikia CCM. Kuteuliwa kwa Mhe. Majaliwa ni kuwapa nafasi watu wa Kanda ya Kusini kujisogeza kimaendeleo na kuonyesha kuwa CCM inawajali na kuwathamini wananchi wa huko na hivyo wananchi wa huko wasahau madhila na vuguvugu la gesi asilia katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

Wawili hawa (Dr. Magufuli na Mhe. Majaliwa) hawakupata nafasi zao kwa bahati mbaya ila ni karata muhimu kwa CCM. Karata hizi zitafanikiwa?
Last edited by Petro E. Mselewa;