Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ndiye aliongoza kwa kuchaguliwa na wapigakura wengi kuliko mbunge yeyote kati ya wabunge 257 waliochaguliwa katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu.
Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), wabunge waliochaguliwa majimboni hadi sasa ni 257 kati ya 264. Majimbo saba hayajafanya uchaguzi kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo vifo vya wagombea na uhaba wa vifaa.
Mbilinyi ambaye pia anafahamika kwa jina la Sugu, alichaguliwa kwa kura zaidi ya 100,000 kati ya 166,256 zilizopigwa.
Taarifa ya NEC inaonyesha orodha ya wabunge waliochaguliwa na idadi ya kura zao, kati ya 10 walioongoza, saba wametoka vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na waliosalia ni wa CCM.
Katika uchaguzi huo, Sugu alifanikiwa kupata kura 108,566 akiwaachia mbali wapinzani wakigawana kura 57,690.
Katika uchaguzi wa mwaka huu, Abdallah Chikota wa Jimbo la Nanyamba (CCM) ndiye pekee aliyepita bila kupingwa.
Kati ya wabunge waliopigiwa kura nyingi, wamo wanawake wawili na wanaume wanane.
Wanawake walioingia 10 bora ni Halima Mdee wa Kawe (Chadema) na Bonnah Kaluwa wa Segerea (CCM) wote kutoka Dar es Salaam.
Licha ya wanawake hao, jiji hilo linaongoza kutoa wabunge wengi waliopigiwa kura nyingi likiwa na majimbo sita likifuatiwa na Arusha lenye majimbo mawili, Mbeya na Morogoro yenye jimbo moja kila mkoa.
Wabunge wengine waliovuna kura nyingi ni Ally Abdallah wa CUF (Temeke) aliyepata kura 103,231; Abdul-Aziz Abood wa CCM (Morogoro Mjini) 99,748; Mdee 96,432 na Kaluwa kura 94,640.
Wengine ni Gibson Olemeiseyeki wa Arumeru Magharibi (Chadema) 94,354 na Mwita Waitara wa Ukonga (Chadema) kura 90,478.
Pia, wamo Saed Kubenea wa Ubungo (Chadema) 87,666; Ali Mangungu wa Mbagala (CCM) 87,249 na Joshua Nassari wa Arumeru Mashariki (Chadema) 86,694.
Waliopata kura chache ambazo hazikufika hata 20,000 katika uchaguzi huo wa Oktoba 25 mwaka huu ni Mwita Boniface wa Bunda Chadema) 12,512; Hamidu Jumaa wa Pangani (CCM) 12,551 na Kizito Joseph wa Madaba (CCM) 12,736. Pia, wamo Edwin Sannda wa Kondoa Mjini (CCM) 13,333 na Hamidu Bobali wa Mchinga (CUF) kura 14,776.
Wengine ni Mary Chatanda wa Korogwe Mjini (CCM) 16,690; Vedasto Ngombale wa Kilwa Kaskazini (CUF) 16,724 na Jerome Bwanausi wa Lulindi (CCM) 17,715.
Pia, wamo Abuu Hamoud wa Kibaha Vijijini (CCM) 18,521 na Cosato Chumi wa Mafinga Mjini (CCM)aliyepata kura 18,594.
Katika uchaguzi huo wapigakura 15,589,639 waliwapigia kura wabunge hao.