Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa imesema imeanza kutekeleza agizo la Rais John Magufuli kwa haraka kama jeshi juu ya kuiwakilisha Serikali katika masuala mbalimbali nje ya nchi baada ya kusitishwa safari za nje kwa maofisa wote wa ndani.
Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Balozi Liberata Mulamula alisema jana kuwa atawapelekea mwongozo mabalozi wote kutekeleza majukumu hayo kwa kasi inayoendana na Serikali ya Awamu ya Tano.
Wiki iliyopita, Rais Magufuli alitangaza kufutwa kwa safari za nje kwa maofisa wake na kusema kuwa safari nyingi zielekezwe vijijini kuwahudumia wananchi na kwamba kazi za nje zifanywe na mabalozi ili kupunguza matumizi ya Serikali.
Hata hivyo, Balozi Mulamula alisema utekelezaji wa agizo hilo la Rais utachukua muda kidogo kutokana na balozi nyingi kukosa rasilimali fedha na wataalamu wa kutosha kufanikisha malengo hayo kwa ufanisi na tayari wameshamweleza tatizo hilo.
“Kwa sasa ikitokea unawaagiza mabalozi wakawakilishe kwenye kongamano la biashara, hatuna maofisa wa biashara wa kutosha au ikitokea kuna kongamano la nishati sisi hatuna wataalamu hao.
“Pia, uteuzi wa mabalozi nao itabidi uwe makini kuhakikisha balozi anayeteuliwa eneo husika ana uwezo wa kutosha kufanya kazi,” alisema.
Akizungumza katika hafla ya miaka 40 ya ushirikiano wa Tanzania na EU, Balozi wa umoja huo, Filiberto Sebregondi alisema wametumia Euro 3 bilioni sawa na Sh6.93 trilioni katika miradi mbalimbali ya maendeleo nchini ambazo zilielekezwa zaidi katika sekta za miundombinu, elimu, usambazaji umeme vijijini, maji, utawala bora na utetezi wa haki za binadamu.
Balozi huyo ambaye pia aliaga jana baada ya kumaliza muda wake, alisema EU itaendelea kusaidia Tanzania miradi ya maendeleo katika nchi ambayo ni mfano wa kuigwa Afrika katika kulinda amani, utulivu na demokrasia.
“Uchaguzi uliopita pamoja na kuonyesha ushindani mkubwa, umeonyesha utulivu wa hali ya juu kwa Watanzania. Hivyo, tunasubiri kuona hali inayoendelea Zanzibar inatatuliwa kwa mazungumzo na kwa kuheshimu matakwa ya Wazanzibari,” alisema Sebregondi.
12 Nov 2015
New