Nape Nnauye Alifungia Milele Gazeti la Mawio - MULO ENTERTAINER

Latest

16 Jan 2016

Nape Nnauye Alifungia Milele Gazeti la Mawio

Serikali kupitia Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nauye, imelifungia kwa muda wote gazeti la kila wiki la MAWIO linalochapishwa na kampuni ya Victoria Media Services Ltd.
Katika tangazo lake lililotolewa kupitia gazeti la Serikali notisi namba 55 ya Januari 15, 2016 Serikali imebainisha kuwa imechukua uamuzi huo wa kulifungia gazeti la Mawio kwa muda wote kwa mujibu wa mamlaka iliyonayo kupitia sheria ya magazeti ya mwaka 1976 sura ya 229 kifungu cha 25(1).
“Mawio linatakiwa kusimamisha uchapishaji wake kwa kipindi chote ikiwemo pia katika vyombo vya mawasiliano vya kielektroniki kuanzia Januari 15, 2016”, ilisema sehemu ya tangazo hilo ambalo limetolewa katika gazeti la serikali, likisainiwa na waziri Nape Nauye.
Tangazo hilo halikuweza kufafanua zaidi ni makosa gani hasa yaliyosababisha gazeti kufungwa na kwanini adhabu iliyotolewa ni kubwa sana ukizingatia kuwa Mawio halikuwahi kufungiwa wala kuonywa kwa kosa lolote katika siku za wa awali.
Serikali ilianza kulikabili rasmi gazeti la Mawio 31 Desemba, 2015 kwa barua iliyoandikwa na msajili wa magazeti ikimtaka mhariri wa gazeti hilo kutoa maelezo ya kwanini gazeti hilo lisifungiwe kufuatia makala zake mbili zenye vichwa vya habari “Hosea kortini” na “Seif Rais Zanzibar” ambazo zilidaiwa kuzua taharuki.
“Nakujulisha kwamba ofisi ya msajili wa magazeti haijaridhika na utetezi wako kwa kuwa hujatoa uthibitisho usio na shaka juu ya madai ya makala ulizochapisha,”ilitamka sehemu ya barua iliyosainiwa na Raphael Hokororo, kwa niaba ya msajili.
Gazeti la Mawio ambalo huandika habari za kiuchunguzi limefuata mkondo uleule ambao gazeti la MwanaHALISI liliufuata 30 Julai 2012 pale lilipofungiwa kwa muda usiojulikana kwa madai ya kuchapisha taarifa za uchochezi.
MwanaHALISI lilikaa kifungoni kwa zaidi ya miaka mitatu kabla ya kurejeshwa kwa amri ya Mahakama Kuu mwezi Agosti, 2015 kufuatia Mkurugenzi wa kampuni ya Hali Halisi Publishers, Saed Kubeneakufungua kesi, akipinga kufungiwa kwa gazeti hilo.